Mlimani Park ‘Sikinde’, Msondo Ngoma kutunishiana misuli leo

Mtanzania - - Hadithi - Maoni yalete hapa 0714288656 Na VALERY KIYUNGU

KATIKA safu hii ya Old Skul, leo tunaangazia mpambano wa bendi kongwe nchini za Mlimani Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ na Msondo Ngoma, bendi hasimu zitakazotunishiana misuli leo kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Mpambano huo, ambao umekuwa gumzo karibu kila pembe ya nchi, unaratibiwa na mdau wa muziki wa dansi, Abdul Fareed Hussein, huku likiwa limepewa jina la Nani Zaidi, lengo likiwa ni kujitathmini uwezo wa bendi hizo mbele ya mashabiki wao.

Kwa kiasi kikubwa mpambano huo umekuwa na majigambo baina ya mashabiki wa pande zote mbili, huku kila upande ukitamba kuwa bendi anayoshabikia, itaifunika bendi pinzani kwa kupiga nyimbo nzuri.

Mpambano huo unafuatia utaratibu waliojiwekea viongozi wa Msondo na Sikinde wa kufanya maonyesho ya pamoja kila baada ya miezi kadhaa, ili kupima uwezo wa bendi zao na mara nyingi yamekuwa yakifanyika katika Sikukuu za kidini kama vile Krismasi na Iddi.

Onyesho hilo, licha ya kuwa linahusisha bendi na wanamuziki wake, ila macho na masikio ya wengi huwa yanawatazama magwiji wawili wa muziki huo, ambao ni Shaaban Dede na Hassan Bitchuka.

Hii imetokana na ukweli kwamba, hao ndio waliobobea zaidi katika utunzi na uimbaji wa nyimbo zenye msisimko na maadili.

Wanamuziki hao wawili leo wanatarajia kuongoza jahazi kwa kila mmoja kuibeba bendi yake ili iweze kuibamiza bendi pinzani, huku wakilenga kuwapa burudani tosha mashabiki wa bendi zao watakaofurika ukumbini hapo kushuhudia.

Miongoni mwa nyimbo za Sikinde ambazo zinatarajiwa kuwa kivutio katika onyesho hili la leo ni Fikirini Unisamehe na Neema, ambazo ziliweza kumpandisha chati Bitchuka miaka kadhaa nyuma.

Kwa upande wa bendi ya Msondo, mashabiki wanatarajia kupata burudani kupitia nyimbo nyingi, mfano Maisha ni Vita, Jane na Fatuma, ambazo Dede aliimba akiwa na bendi tofauti alizowahi kujiunga nazo. Wakizungumza na safu hii kwa nyakati tofauti hivi karibuni jijini Dar es Salaam, viongozi wa bendi za Sikinde na Msondo mbali na kujinasibu, walisema kuwa bendi zao zimejiandaa vya kutosha kuweza kutoa burudani safi leo kwa mashabiki ambao watafika ukumbini kushuhudia mtanange wao. Abdallah Hemba, kiongozi wa bendi ya Mlimani Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ alisema bendi yake kwa wiki kadhaa ilikuwa imeweka kambi maalumu ili kuiangamiza Msondo Ngoma.

“Sikinde tumefanya maandalizi makubwa kuhusiana na onyesho la kesho (leo), tumekuwa kambi maalumu ya kuwamaliza Msondo, pia tumetunga nyimbo mpya ambazo sitaweza kuzitaja,” alitamba Hemba, ambaye pia ni mtunzi na mwimbaji wa Sikinde.

Naye Juma Katundu, ambaye ni kiongozi wa jukwaa wa bendi ya Msondo Ngoma, alisema bendi yake katika onyesho hilo imeandaa nyimbo kali ambazo zitaweza kuwaburudisha mashabiki na kuibamiza Sikinde. “Msondo tumepata ‘ushindi’ tangu juzi, kwani matokeo ya onyesho hilo tayari tumeyapata, Sikinde watakuwa wanakamilisha ratiba, lakini hawana chao,” alisema Katundu, ambaye pia ni mtunzi na mwimbaji wa kutumainiwa wa Msondo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.