Rais mpya Iran kujulikana leo

Mtanzania - - Kimataifa -

U CHAGUZI wa urais nchini Iran ulioanza jana unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku kukiwa na matumaini mshindi wa kiti hicho kuanza kujulikana leo.

Vituo vya kupigia kura 63,000 vilifunguliwa jana asubuhi nchini humo, huku wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakisema kuchaguliwa au kutochaguliwa tena kwa Rais wa sasa, Hassan Rouhani, kunaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa siyo tu za ndani ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu, bali na za kimataifa.

Jumla ya wapigakura milioni 54 walio na haki ya kupiga kura, pamoja na kuwepo kawaida ya wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura, matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa leo.

Uwezo wa Iran wa silaha za kinyuklia na umuhimu wa kimkakati ulio nao nchi hiyo katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, ni masuala mawili makuu yanayozingatiwa wakati wa kupiga kura leo kuwachagua wagombea wafuatao:

Hassan Rouhani

Ni msomi wa kidini na mwanasheria mwenye umri wa miaka 68 na ndiye rais aliyepo madarakani kwa sasa. Rouhani anatazamwa kama mwanamageuzi wa misimamo ya wastani, na ni mmoja wa wagombea wawili wanaoongoza katika kinyang’anyiro hicho cha urais, akifuatiwa na Ebrahim Raisi.

Wakati wa muhula wake wa kwanza, Rouhani alifungua milango ya nchi hiyo na kuzikaribisha nchi za Magharibi, alisimamia makubaliano ya 2015 ambayo yaliihitaji Iran kupunguza uwezo wake wa kinyuklia, ili nchi za Magharibi kwa upande wake zipunguze vikwazo vya kimataifa ilivyoiwekea nchi hiyo.

Rouhani ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa tena, ataendeleza mahusiano ya kidiplomasia na kuvutia uwekezaji wa kimataifa nchini Iran.

Ebrahim Raisi

Kiongozi wa kidini mwenye umri wa miaka 57, ambaye anatazamwa kama mshirika wa karibu na anayeweza kumpokea madaraka Kiongozi Mkuu wa Kidini, Ali Khamenei. Ingawa Raisi hataki kusitisha makubaliano ya kinyukilia yaliyofikiwa mwaka 2015, lakini amesema Iran inapaswa kujitenga kisiasa na kiuchumi kutoka nchi za Magharibi. Raisi pia anapinga uwekezaji zaidi wa kigeni.

Mostafa Mirsalim

Ni mgombea mwingine wa tatu ambaye aliwahi kuwa waziri wa utamaduni na anatazamwa kama mtu mwenye misimamo mikali ya kihafidhina. Nafasi yake ya kushinda katika uchaguzi huu inatarajiwa kuwa ni ndogo sana.

Mostafa Hashemitaba

Mgombea huyo ana umri wa miaka 76 na mwenye misimamo ya kisiasa ya wastani, aliwahi kuwa makamu wa rais kuanzia 1997 - 2005 chini ya uongozi wa Mohammad Khatami, mwanamageuzi wa kwanza kuwahi kuwa rais nchini humo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.