SOPHIA MSETTI ‘MATTY’

Kocha anayechipukia kuzalisha vipaji vya soka

Mtanzania - - Michezo - Na ZAINAB IDDY,

WAKATI wadau wa soka wakiamini Tanzania makocha wengi wenye weledi wa mpira ni wanaume, hali ni tofauti kwa sasa. Wapo makocha wanawake ambao nao wamejitosa katika taaluma ya ukocha ili kusaidia kukuza soka la vijana wa Tanzania, akiwamo mwanadada Sophia Msetti, maarufu Matty. Kocha huyo aliwahi kuwa mchezaji wa timu za wanawake za Sayari Queens, Vijana Queens pamoja na timu ya Wanawake ‘Twiga Stars’. Matty kwa sasa anafundisha timu za watoto kuanzia umri wa miaka 5 hadi 15 kwenye Shule ya Maget Youth Soccer, iliyopo Mbezi, jijini Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, katika ofisi za New Habari (2006) LTD, zilizopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam, Matty anasema sababu za kuingia kwenye soka, licha ya wazazi wengi kuwakataza watoto wao, ni ushawishi alioupata kutoka kwa baba yake mzazi, Joseph Msetti, ambaye ni Mwenyekiti wa timu ya Tegeta United. “Baba yangu ni mtu wa mpira sana na mara nyingi anapomaliza shughuli zake za kila siku, anapenda kwenda kwenye viwanja vya mpira kufanya mazoezi, jambo ambalo nilikuwa nalipenda. “Kitendo cha kwenda mara kwa mara kwenye mazoezi na baba kilinifanya niweza kufahamu baadhi ya mambo yanayohusu soka na mwisho nikajikuta naingia uwanjani kucheza na hata kufikia hatua ya kufanya kazi ya ukocha,” anasema. Anasema kuwa, alianza fani ya ukocha baada ya kucheza kwenye timu ya Sayari Queens na Vijana Queens, ndipo alianza kutamani kusomea masuala ya ukocha.

“Kwa mara ya kwanza niliitwa kwenye timu ya taifa ‘Twiga Stars’ mwaka 2006 -2010, iliyokuwa chini ya kocha Seleman Gwaje, ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Tangu nilipoitwa Twiga Stars nikaanza kupenda soka na baada ya kutoka kwenye timu hiyo, nikaanza kufuatilia njia za kutaka kusomea ukocha, lakini mwaka 2012 nilianza kufundisha kwa kutumia uzoefu nilioupata nikiwa mchezaji,” anasema.

Anasema kuwa, baada ya kusubiri kwa muda mrefu, alipata mafunzo ya kozi ya ukocha ngazi ya awali (Preliminary), iliyomalizika Mei 15, mwaka huu, iliyoendeshwa na Chama cha Soka Manispaa ya Ubungo (UFA). Malengo yake: Anasema malengo yake makubwa ni kuwa kocha wa kusaidia kuzalisha vipaji vya vijana na kuviendeleza kwa faida ya taifa kwa ujumla.

“Kwa hapa nchini makocha wa kiume ndio wanaoonekana kujitoa katika kuzalisha au kuendeleza vipaji vya watoto, hivyo ujio wangu ni kuwaonyesha hata wasichana au wanawake tunaweza.

“Nashukuru Mungu hadi sasa najivunia mtoto mmoja anayeitwa Aron, aliyepata nafasi ya kusomeshwa bure nchini Afrika Kusini, aliyetoka kwenye mikono yangu katika shule ninayofundisha,” anasema. Anasema kuwa, bado hajakata tamaa na kwamba ataendelea kusomea zaidi taaluma hiyo ili kuongeza maarifa zaidi.

“Kwa kweli nashukuru kwa hiki nilichojifunza na nitaendelea kusoma kozi za ukocha kwa kadiri Mungu atakavyonijalia ili niweze kutimiza malengo yangu ya kuwa kocha,” anasema.

Anasema anatamani kuwa kama kocha Juma Masanywa, aliyekaa Marekani kwa miaka 18 akifundisha vijana.

taifa y a

VIPAJI: Matty (wa tatu kushoto), akiwa na vijana wake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.