Mbio za baiskeli kufanyika kesho

Mtanzania - - Michezo - Na JACKLINE LAIZER

MASHINDANO ya wazi ya mbio za baiskeli yanatarajiwa kufanyika

keshokutwa, huku mikoa zaidi ya saba ikitarajiwa kushiriki mashindano hayo.

Mashindano hayo yameandaliwa na Klabu ya waendesha baiskeli ya Arusha Cycling Club (ACC), huku yakidhaminiwa na Kampuni ya Habari Node Ltd.

Akizungumza mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Klabu ya ACC, Moses Andrew, alisema mashindano hayo yana lengo la kuhamasisha mchezo wa baiskeli na kuzalisha vipaji vipya.

“Ili mchezo wa baiskeli uweze kufanya vizuri na kujulikana zaidi, lazima mashindano ya mara kwa mara yafanyike, kwani itamsaidia mchezaji kujua kiwango chake kikoje na vile vile mchezo utazidi kupiga hatua,” alisema Andrew. Alisema mbio hizo zitahusisha wanaume na wanawake, ambapo zitakimbiwa katika makundi matatu, ambayo ni wanaume wakubwa watakimbia km 120, wanawake, wazee na watoto watakimbia km 70.

“Tumekuwa tukiandaa mashindano haya mara kwa mara ili kuweza kuuhamasisha mchezo huu wa baiskeli na kuzalisha vipaji vipya, vilevile kuwataka wadau kujitokeza kuunga mkono mchezo huu,” alisema Andrew.

Alisema wanaishukuru Kampuni ya Habari Node, ambayo imekuwa ikiwaunga mkono kwa kuwadhamini mara kwa mara.

Alitaja zawadi za washindi wa km 120 ambao ni wa kwanza mpaka kumi na washindi wa km 70 washindi watakuwa ni wa kwanza mpaka wa tatu, huku zawadi hizo zikiwa ni fedha taslimu.

Aliitaja mikoa itakayoshiriki mashindano hayo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Iringa, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.

Mashindano hayo yataanzia katikati ya jiji la Arusha, sehemu ya Mnara wa saa kuelekea barabara ya Makuyuni na zitaishia katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.