Serengeti Boys ‘yawaondoa’ wabunge bungeni

Mtanzania - - Michezo - Na RAMADHAN HASSAN

WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juzi waliikacha Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na kukimbilia katika mgahawa wa Bunge ili kushuhudia mchezo kati ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boy’ dhidi ya Angola.

Pia jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni, wabunge waliipongeza timu hiyo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Angola.

Timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Taifa ya Angola kwa mabao ya Kelvin Nashon Naftal na Abdalah Hamis Seleman.

Wabunge hao, ambao walikuwa wakiongozwa na Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM) na Cosato Chumi wa Mufindi Mjini (CCM), walikuwa wakiishangilia timu hiyo kwa nguvu.

Wakati mchezo huo ukiendelea, wabunge hao walikuwa makini, huku Chumi akionekana kukoshwa zaidi na uchezaji wa wachezaji hao.

Baada ya mshambuliaji wa Serengeti Boys, Suleiman kufunga bao la pili, wabunge hao walianza kushangilia kwa nguvu, hali iliyowalazimu askari waliokuwapo eneo hilo kuwakataza kushangilia.

Wakizungumza jana asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu, wabunge hao waliipongeza timu hiyo kwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.