Funga kazi Ligi kuu Tanzania bara

Mtanzania - - Michezo -

Wanajangwani kukabidhiwa kombe kwa msimu wa tatu mfululizo.

Katika mchezo huo wa leo, Yanga huenda ikawakosa wachezaji Donald Ngoma, Kelvin Yondan na Simon Msuva, ambao walipata majeraha kwenye michezo iliyopita.

Mbao wao wanahitaji ushindi dhidi ya Yanga ili kusalia kwenye ligi msimu ujao, kutokana na kujikusanyia pointi 30.

Matokeo ya ushindi pekee ndiyo yataweza kuiokoa Mbao, ambayo pia italazimika kuziombea mabaya baadhi ya timu zilizopo kwenye nafasi za chini ili yenyewe iweze kubaki msimu ujao.

Vita ipo katika timu mbili zinazotakiwa kuungana na JKT Ruvu kushuka daraja msimu huu na mchuano huo unaanzia kwa timu zilizoshika nafasi ya 11 hadi 15 kwenye msimamo wa ligi hiyo. Vita hiyo itakuwa katika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, itakayozikutanisha Majimaji iliyopo na pointi 32 kuwakaribisha Mbeya City, wenye uhakika wa kusalia kwenye mashindano hayo msimu ujao.

Timu nyingine ni African Lyon, yenye pointi 31 wanaohitaji ushindi ili kubaki kwenye ligi, watamaliza ngwe yao ugenini kwa kucheza dhidi ya JKT Ruvu.

Ndanda wao wana kibarua kigumu mbele ya JKT Ruvu, ambayo tayari imeshashuka daraja hadi sasa, na ili wabaki watatakiwa kupigana ili kupata pointi tatu muhimu.

Kwa upande wao Toto Africans, waliotoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Yanga, nao wanakabiliwa na wakati mgumu, kwani pointi 29 walizojikusanyia hadi sasa ni kama wameshashuka daraja kutokana na pointi hizo kutokuwa na uzito mkubwa kama ilivyo kwa Mbao, Lyon na Majimaji.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo, Azam FC itaikaribisha Kagera Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, wakati Ruvu Shooting ikiwa ugenini Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kuwavaa Stand United.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.