MOURINHO: Sitafanya makosa msimu ujao

Mtanzania - - Michezo -

KOCHA wa timu ya Manchester United, Jose Mourinho, amesisitiza kwamba hatafanya makosa msimu ujao, kwa sababu sasa anaifahamu vema timu hiyo.

United inaweza kumaliza msimu huu ikiwa na mataji makubwa mawili endapo itaifunga Ajax kwenye mchezo wao wa fainali ya Ligi ya Ulaya, baada ya hivi karibuni kushinda Kombe la Ligi.

Kwa sasa United wanapambana kwenye Ligi Kuu England, hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kumaliza ligi hiyo wakiwa nafasi ya sita, licha ya ushindi watakaoupata dhidi ya Crystal Palace kwenye mchezo wa kesho.

Endapo United watanyakua ubingwa wa Ligi ya Ulaya, watapata nafasi ya moja kwa moja kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Mourinho alisisitiza kwa kawaida msimu wa kwanza huwa mgumu, lakini anajipanga kufanya makubwa kwenye msimu ujao wa 2017/18, baada ya kujifunza mambo mengi msimu huu.

“Najaribu kuchambua ukweli kabla ya kutua kwenye klabu hii, lakini utakapokuwa ndani ya klabu husika ndipo utakapofaham ukweli halisi,” alisema Mourinho.

“Ukiwa nje ya klabu unaweza kufikiri kwamba unawafahamu vizuri wachezaji, lakini si kweli, utawafahamu tu endapo utakuwa nao karibu kwenye kipindi kizuri.

“Kitu ninachofarijika ni kitendo cha kutoka kwenye msimu wa kwanza na kuingia wa pili,” alisema Mourinho.

Lakini Mourinho anaeleza kuwa, anajihisi mwenye furaha baada ya kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwenye Bodi ya United, wakati ambao anaelekea kwenye kipindi cha usajili ili kukiimarisha kikosi chake msimu ujao.

“Kila siku nina maswali kuhusu kitu kilichowafanya Manchester United kushindwa kupata mafanikio katika miaka mitatu iliyopita.

“Jibu moja ni uhalisia wa Ligi Kuu, nguvu ya uchumi kwa klabu nyingi pamoja na uimara ambao klabu inakuwa nayo, kutokana na ukweli huo, kuna kazi ya kufanya kwa kikosi cha United, jambo zuri ni kwamba klabu inafahamu, bodi pia na tupo pamoja kulifanikisha jambo hilo,” alisema Mourinho.

Mourinho

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.