Xavi awatahadharisha Madrid

Mtanzania - - Michezo -

MCHEZAJI wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, ameitahadharisha Real Madrid kuwa Malaga si timu rahisi na kuifunga kwenye uwanja wao wa nyumbani ni kazi ngumu.

Madrid sasa wanahitaji pointi moja tu kutwaa ubingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano, mchezo wao wa mwisho dhidi ya Malaga wanatarajia kucheza kesho wakiwa ugenini wakati Barcelona wakivaana na Eibar.

Hata hivyo, Madrid wanapewa nafasi kubwa kuifunga Malaga, lakini Xavi anaamini mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na kiwango safi cha timu ya kocha Michel Getafe, ambayo imefungwa mechi moja tu katika nane za mwisho.

“Malaga wapo katika kiwango bora na kupata ushindi kwenye uwanja wao si kazi rahisi, hivyo naona dhahiri jinsi Michel atakavyoisaidia Barca, lakini tunahitaji siku ya mwisho kama ile ya Tenerife miaka kadhaa iliyopita kwa Barca kutetea taji lao msimu huu.

“Kipigo kama kile cha Alaves katika uwanja wa Camp Nou na Deportivo katika uwanja wa Razor vimeipa Barcelona mlima mkubwa wa kupanda kuelekea mwisho wa msimu huu,” alisema Xavi.

Wakati Xavi akiendelea kuiombea mema timu yake ya zamani, anakiri kuwa itakuwa ni pigo kubwa kwa Madrid ikiwa hawatatwaa taji hilo msimu huu.

“Sidhani kama Real Madrid wataiachilia fursa ya kutwaa taji iyeyuke kirahisi ilhali wakiwa imara na thabiti msimu wote huu,” alisema Xavi na kuongeza mechi dhidi ya Celta Vigo ilikuwa muhimu kupata ushindi na kuifanya Madrid kuwa karibu kunyanyua taji hilo.

“Naomba wafungwe na Malaga na Barca washinde taji, lakini naona si jambo rahisi kabisa, Madrid wana wachezaji mahiri kama Kroos, Modric na Isco.”

Xavi alisema bado bingwa hajajulikana, lakini hakuna aliyetarajia Tenerife wangeifunga Madrid 1992 na 1993.

“Huo ni ushahidi kuwa siku ya mwisho wa La Liga inaweza kuleta vioja kwa timu kurejea kwenye historia, hivyo bado tumaini linaendelea,” alisema Xavi.

Xavi Hernandez

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.