Serikali yakana uhusiano na Korea Kaskazini

SERIKALI imekanusha kuwa na uhusiano wa aina yoyote ile, ukiwamo wa kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa au kijeshi na nchi ya Korea Kaskazini, iliyowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (UN).

Mtanzania - - Mbele - Na EVANS MAGEGE

Ripoti ambayo Baraza la Usalama limeipata imepitwa na wakati. Na sisi tutawajibu na kueleza, ndiyo maana mimi nimewaita mabalozi wakubwa wa kudumu wa Baraza la Usalama (Uingereza, Marekani, China, Urusi na Ufaransa), kuwaeleza kwamba ripoti hiyo si sahihi.

SERIKALI imekanusha kuwa na uhusiano wa aina yoyote ile, ukiwamo wa kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa au kijeshi na nchi ya Korea Kaskazini, iliyowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (UN).

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya hivi karibuni ya Baraza la Usalama la UN, inayoituhumu Tanzania kukiuka vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Korea Kaskazini.

Dk. Mahiga alisema ripoti hiyo imeituhumu Tanzania kuendeleza uhusiano wake na Korea Kaskazini katika mambo fulani ambayo hakutaka kuyataja.

Alisema UN imeiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa, kijeshi na mawasiliano ya kila aina ili kuitenga nchi hiyo, baada ya kukiuka agizo la kusitisha utengenezaji na majaribio ya silaha za nyuklia.

“Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekata uhusiano na Korea Kaskazini. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitumia wataalamu wake, wametoa taarifa inayodai kwamba Tanzania ni kati ya nchi 11 ambazo zina uhusiano wa karibu na Korea Kaskazini na katika uhusiano huo tunakwenda kinyume na uamuzi wa baraza hilo la kuiwekea vikwazo vya kila aina Jamhuri ya Korea Kaskazini.

“Sisi tumetajwa kwamba tuna uhusiano ambao huko nyuma tulishawahi kutajwa pia tuna uhusiano wa kuwaruhusu Korea Kaskazini na kampuni zao kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye meli zao.

“Ni kweli kwamba huko nyuma tumewahi kuwa na uhusiano, wamekuwa wanafadhili baadhi ya hospitali hapa nchini, tumekuwa na uhusiano wa kibiashara, hasa kwa vifaa vya ulinzi na usalama wa nchi yetu, sasa hivyo wao wanaona vinakiuka uamuzi wa Baraza la Usalama,” alisema.

Dk. Mahiga alisema siku za nyuma zilipoibuka tuhuma za meli za nchi hiyo kupeperusha Bendera ya Tanzania, Serikali ilichukua hatua na kuhakikisha zinatambulika popote na kufuta usajili wake, hivyo bendera zikashushwa.

“Baada ya hatua hiyo tulipeleka taarifa UN kwamba tumefanya hilo, lakini nakiri kwamba uhusiano wa kidiplomasia huko nyuma tulikuwa nao, walitujengea sehemu mbalimbali, lakini tulisitisha uhusiano wa kidiplomasia, ingawa bado kuna ubalozi hapa nchini, hivyo naweza kusema uhusiano wa kidiplomasia upo katika ngazi ya chini mno.

“Badala yake tuna uhusiano wa karibu na Korea Kusini. Na Korea ya Kusini imeichangia Tanzania kama moja ya nchi ambazo zinapewa misaada mingi zaidi katika Bara la Afrika,” alisema.

Pia alisema Tanzania haikuchukua uamuzi huo kwa sababu ya kushinikizwa, bali ni kutokana na imani kwamba, kuwapo kwa silaha za maangamizi ni tishio kubwa kwa amani si tu ya Peninsula ya Korea, ila ni tishio la amani duniani.

Alisema Tanzania haina ugomvi na Korea Kaskazini, lakini kitendo cha nchi hiyo kutengeneza silaha za maangamizi si kizuri kwa heshima ya ustaarabu na usalama duniani na kwa kutambua hilo, serikali ikaanza kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza uhusiano kwa lengo la kuhakikisha vikwazo vya UN vinazidi kuwabana.

“Kama ni meli, kama ni misaada tulipunguza, lakini pia tulikuwa na uhusiano wa kibiashara na Kampuni za Korea Kaskazini kusaidia vitu fulani kwenye kuunda jeshi letu na kutengeneza vitu fulani ambavyo tunahitaji kwa ulinzi na usalama wa jeshi letu.

“Wakaanza kusema na huko nako acheni kabisa, sasa ule uamuzi ukitolewa wanatarajia siku hiyo ndani ya saa 24 unaacha. Lakini hata hivyo sisi tulifanya kiungwana, tukasema tutatengeneza utaratibu wa kuweza kuondoa huo uhusiano na mwaka 2014 tukawaambia sisi tumepunguza uhusiano wa kijeshi na Korea Kaskazini, vitu hivi vina mikataba yake na tumeishaamua kufanya hivyo,” alisema.

Pia alisema katika ripoti ya Baraza la Usalama iliyoandikwa Septemba 5, mwaka huu, haikuzungumzia meli, bendera, misaada ya hospitali au uhusiano wa kidiplomasia, bali imedai kwamba Tanzania bado inaendelea na uhusiano katika kukarabati na kurekebisha vifaa fulani.

“Imebidi tuwafafanulie kwamba mara nyingi hizi ripoti zinapoandikwa na hao wataalamu inaweza ikaandikwa leo, lakini inakuja kufikishwa kwenye Baraza la Usalama baada ya miezi 12 au 18.

“Ripoti ambayo Baraza la Usalama limeipata imepitwa na wakati. Na sisi tutawajibu na kueleza, ndiyo maana mimi nimewaita mabalozi wa wakubwa wa kudumu wa Baraza la Usalama (Uingereza, Marekani, China, Urusi na Ufaransa), kuwaeleza kwamba ripoti hiyo si sahihi.

“Tutajibu hiyo ripoti, mimi nakwenda Umoja wa Mataifa (kesho) na kule nakwenda katika mkutano mkuu wa kila mwaka, lakini nina hakika nitakutana na nimeshaambiwa tutakutana na wawakilishi wa wakubwa wote hao na nitawapa majibu kama haya niliyowapa hapa,” alisema.

– PICHA: IMANI NATHANIEL

MKUTANO: Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya tuhuma za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Korea ya Kaskazini. kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aziz Mlima na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara hiyo, Mindi Kasiga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.