Dereva wa Heche akatwa kwa mapanga

Mtanzania - - Mbele - Na TIMOTHY ITEMBE

WATU wasiofahamika wamemvamia dereva wa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) na kumpora vitu alivyokuwanavyo, ikiwa ni pamoja na hati ya kusafiria.

Hali hiyo imemkwamisha mbunge huyo kwenda Nairobi, nchini Kenya, kumtembelea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, anayetibiwa jijini humo.

Mbali na kumpora vitu mbalimbali, pia wamemjeruhi kwa kumkata na mapanga, hivyo kumsababishia majeraha sehemu za kichwani na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa, Jeshi lake linawasaka waliohusika na tukio hilo ili kuwatia mbaroni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mrimi Zablon, ambaye ni Katibu wa Mbunge Heche, alisema dereva hiyo alishambuliwa Septemba 14, mwaka huu, saa 2 usiku wakati akiwa anatoka nyumbani kwake Mtaa wa Kibasa kwenda nyumbani kwa Mbunge Mtaa wa Mawasiliano, kuchukua gari kwa ajili ya safari ya kwenda Nairobi.

“Mbunge alikuwa na safari ya kwenda Nairobi, nchini Kenya, kwa ajili ya kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye amelazwa huko, sasa akiwa njiani alivamiwa na watu ambao walimpora begi la nguo alilokuwa nalo, simu ya mkononi pamoja na fedha Sh 50,000 baada ya kumshambulia kwa kumkata na mapanga,” alisema Zablon.

Alisema kuwa dereva huyo alidai kuvamiwa na watu wawili ambao hakuwatambua na kufanikiwa kumjeruhi vibaya sehemu za kichwani na kumsababishia majeraha makubwa, lakini alifanikiwa kuwaponyoka na kukimbilia nyumbani kwa Mbunge ambako walimuwahisha katika Hospitali ya Bomani ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu. Mrimi aliongeza kuwa, hali yake inaendelea vizuri, lakini kutokana na kuhitajika kupigwa X-Ray, walilazimika kumsafirisha hadi Wilaya ya Rorya, ambako alikuwa akichukuliwa vipimo na baadaye kurejea hospitalini hapo kwa matibabu zaidi.

“Baada ya kumshughulikia matibabu na afya yake kuonekana ipo katika hali nzuri, Heche ameendelea na safari yake leo (jana) ya kwenda Nairobi kumsalimia Lissu, lakini alilazimika kutafuta dereva mwingine,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.