January: Wafanyabiashara epukeni majokofu ‘vimeo’

Mtanzania - - Habari - Na RAMADHAN HASSAN

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, amewataka wafanyabiashara kuepuka kuingiza nchini bidhaa zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi.

Hayo alieleza jana mjini hapa wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya tabaka la Ozoni.

Waziri Makamba alisema kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ni muhimu ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara.

Waziri Makamba alitoa wito kwa kila mwananchi kushiriki katika kuhifadhi Tabaka la Ozoni.

“Ni lazima kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba) na ambavyo vinatumia vipoozi aina ya Chlorofluorocarbons (R11 na R12),” alisema Makamba.

Aidha, Makamba aliwataka Watanzania kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzimia moto nyenye kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni.

Aidha, alisema mafundi wa majokofu na viyoyozi wahakikishe kuwa wananasa na kutuma tena vipoozo kutoka kwenye viyoyozi na majokofu badala ya kuviacha huru visambae angani.

Waziri Makamba alitoa wito kwa mafundi kutoa elimu kwa wateja wao kuhusu njia rahisi za kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wanavyotumia.

“Serikali imeandaa mpango wa kuondosha kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni jamii ya Hydrochlorofluorocarbons,” alisema Makamba

Alisema mpango huo unaendelea na umetoa mafunzo kwa wakufunzi 35 wa vyuo vya ufundi Veta kuhusu teknolojia mpya za kuhudumia majokofu, viyoyozi na mitambo ya kupoozea.

Pia wametoa mafunzo kwa Watanzania 450 ambao ni maofisa forodha na wasimamizi wa sheria kuhusu kanuni za usimamiziwa mazingira.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.