‘Wahuni’ watano wakamatwa vurugu za Arsenal, Cologne

Mtanzania - - Habari -

MASHABIKI watano wanashikiliwa na polisi, wakihusishwa na vurugu zilizotokea juzi kwenye Uwanja wa Emirates, ambapo wenyeji Arsenal walikuwa wakipepetana na Cologne ya Bundesliga katika mchezo wa Ligi ya Europa.

Mchezo huo ulilazimika kuchelewa kuanza baada ya mashabiki 20,000 wa Cologne kuvamia uwanja, licha ya kuwa ni tiketi 3,000 pekee zilizokuwa zimeuzwa kwa ajili ya wageni hao kutoka Ujerumani.

Taarifa zimedai kwamba, mashabiki wa Cologne waliokuwa wanatoa ishara za kilichokuwa Chama cha Kidikteta nchini humo, Nazi, walifanya vurugu ikiwamo kumwaga mikojo uwanjani hapo. Saa moja kabla ya mtanange huo kuanza na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, mashabiki wa Cologne walionekana mitaaani wakiandamana.

Mashabiki wengi waliokuwa kwenye vurugu hizo ni wale ambao hawakuwa na tiketi, wakitaka kuingia bure kabla ya polisi kuhakikisha hali ya utulivu na mchezo kuanza.

Kwa upande wake kocha Arsene Wenger, amelizungumzia tukio hilo, akisema Shirikisho la Soka (Uefa) linapaswa kulipa uzito. “Wanatakiwa wafanye uchunguzi kujua kilichotokea.

“Kulikuwa na watu wengi kuliko waliokuwa na tiketi. Tumeliacha hilo kwa polisi. Sijui (mashabiki wa Cologne) waliwezaje kuwameza mashabiki wetu. Sijui waliwezaje hilo,” alisema Wenger.

Hata hivyo, kocha Cologne, Peter Stoger, alikataa kuligusia tukio hilo, akisema kazi yake ni kufundisha soka na si kuzungumzia mashabiki wa klabu yake. “Hakuna cha kuzungumzia kuhusu mashabiki,” alisema Stoger. “Mimi ni kocha na kazi yangu ni timu na si mashabiki.”

Kwa upande mwingine, Arsenal watashuka dimbani kesho kumenyana na mahasimu wao wa jijini London, Chelsea, katika mchezo wa Ligi Kuu England utakaochezwa Stamford Bridge na kuchezeshwa na mwamuzi, Martin Atkinson. Blues wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na nguvu ya ushindi wao wa mabao 6-0 dhidi ya Qarabag. Wakati Arsenal juzi ikiwapumzisha Alexandre Lacazette, Laurent Koscielny na Petr Cech, Antonio Conte hakuwatumia Alvaro Morata na David Luiz, hivyo mastaa wote hao watakuwa uwanjani hiyo kesho.

“Tulicheza na Chelsea katika mchezo wa Ngao ya Jamii na Kombe la FA msimu uliopita, kwa hiyo najua tunaweza kuwafunga,” alisema mlinda mlango wa Gunners, Petr Cech.

“Mechi tulizocheza dhidi ya Stoke na Liverpool hazikwenda tulivyotaka. Kiwango kilikuwa kizuri dhidi ya Stoke lakini matokeo yalikuwa ovyo, kwa sababu tulikuwa na nafasi nyingi lakini hatukuzitumia.”

Chelsea wameshinda mechi zao tano zilizopita walizocheza na Arsenal wakiwa Stamford Bridge na vijana hao wa Wenger hawajaweza kuzuia nyavu zao kutikiswa uwanjani hapo katika mechi zote 12 zilizopita.

Akiuzungumzia mtanange wa kesho, kocha wa Chelsea, Antonio Conte, alisema: “Mfumo wetu sikuzote uko hivi, kushambulia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.