Vyama vijipange kupokea mabadiliko

Mtanzania - - Tahariri -

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imevitaka vyama vya siasa na vya kiraia kuwasilisha mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria mpya ya vyama vya siasa ndani ya wiki mbili ili mchakato wake ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu 2020.

Barua ya Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, inavitaka vyama hivyo kutoa mapendekezo ya ziada kuboresha rasimu hiyo kabla ya kujadiliwa na Bunge.

Katika mkutano wa viongozi wa vyama 21 vya siasa na Msajili Jaji Francis Mutungi, kujadili mapendekezo ya sheria mpya itakayofuta Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992, mapendekezo hayo yalipingwa na vyama hivyo vikisema hayakuwa na lengo jema kwao.

Sisi tunaona sheria mpya itavipa vyama vya siasa hasa vile vichanga fursa mpya ya kushiriki katika ujenzi wa taifa kikamilifu kuliko ilivyo sasa ambapo baadhi ya vyama vya siasa vimegeuka kuwa makundi ya kudandia matukio na kuibuka na kuzama nyakati za uchaguzi.

Pia, sheria hiyo inapendekeza kupigwa marufuku kwa vikundi vya ulinzi na usalama vya vyama pamoja na kutoa mafunzo ya nguvu kwa vikundi hivyo. Mtanzania Jumamosi tunaliunga mkono pendekezo hili kwani vikundi hivi vya ulinzi vilikuwa chanzo cha vurugu katika baadhi ya sehemu.

Ni busara nchi ikabaki na vikundi vya ulinzi vile tu ambavyo viko chini ya sheria zinazoeleweka. Nasi tunatoa mapendekezo yetu kwa kuvitaka vyama vikuu vya CCM, Chadema na CUF viwe vya kwanza kuvifuta vikundi vyao vya ulinzi.

Tofauti na sheria ya sasa inayovipa hadhi sawa vyama vyote vyenye usajili wa kudumu isipokuwa katika suala la kupata ruzuku, kutakuwa na utaratibu wa kuvipanga kwenye madaraja; vyenye uwakilishi, visivyo na uwakilishi kabisa na vyenye uwakilishi mdogo. Jambo hili ni jema kwani litakifanya kila chama kutendewa haki kwa jinsi ambavyo kinakubalika na wananchi.

Tunasema sheria mpya itavipa vyama vya siasa hasa vidogo, changamoto ya kutumia muda wao kunadi sera zao kwa wananchi ili wakubalike kuliko kutumia muda mwingi kulalamika na kuilaumu Serikali iliyoko madarakani.

Ingawa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanalalamikia vifungu hivyo wakisema si rafiki katika ukuzaji wa demokrasia nchini, tunadhani sasa ni muda mwafaka wa kuibadili sheria ya awali kwani imedumu kwa miaka 25.

Pengine katika vifungu vinavyowapa shida baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ni pendekezo jipya la ukomo wa kukaa madarakani kwa viongozi wa vyama na adhabu kwa viongozi wanaokiuka Katiba.

Hili lazima litazamwe kwa umakini. Ni jambo bora kubadili viongozi wa vyama vya siasa kila baada ya miaka mitano lakini wadau ni vyema wakafikiria namna ya kufanya pale wapenzi na wanachama wanapokuwa bado wanataka kuongozwa na kiongozi wa zamani. Hili tunalisema kwa vyama vichanga. Kumbuka hata vyama ambavyo ni vikubwa sasa viongozi wao wa awali walitumia muda mwingi kuvilea hadi vikakua.

Badala ya kulalamika tu ni vyema wadau wa siasa wakajitokeza kwa wingi kutoa maoni yao ili baadaye nchi ipate sheria bora zaidi ya jinsi ya kuendesha vyama vya siasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.