Msafiri Zawose ameonyesha muziki wa asili ni dili

Mtanzania - - Tahariri - Na CHRISTOPHER MSEKENA

LICHA ya Tanzania kutomfahamu sana msanii wa muziki wa asili nchini, Msafiri Zawose, dunia inamtambua na kumpa heshima kubwa ambayo huenda hakuipata hapa nyumbani kutokana na mashabiki wengi wenye nguvu, hasa vijana kuupa nafasi muziki wa Bongo Fleva.

Msanii huyu wa muziki wa asili amepewa heshima kubwa na tuzo za Africa Magazine Music Awards (AFRIMMA 2017) za nchini Marekani katika kipengele cha Msanii Bora wa Muziki wa Asili barani Afrika, akichuana na wasanii wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Yeye amekuwa Mtanzania pekee kwenye tuzo hizo za mwaka huu ambapo anahitaji kura yako kama Mtanzania na mpenzi wa muziki nchini kupitia wavuti ya tuzo hizo ambayo ni www.afrima.com na ataweza kuibuka mshindi na kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu.

Wengi tumekuwa hatumfahamu Msafiri kwa sababu tumewekeza nguvu nyingi kwenye Bongo Fleva, ambayo kwa sasa inafanya vizuri, ni jukumu letu sasa kuwekeza nguvu hizohizo katika aina nyingine za muziki, ukiwamo huu wa asili, ili tuendelee kupata matokeo chanya kwenye tasnia.

Msafiri Zawose ni mtoto wa marehemu Dk Hukwe Zawose, ambaye ni mwasisi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo, ambaye alimwongoza na kumpa mbinu za kiufundi na kitaaluma kuhusu muziki wa asili na matokeo yake tunaanza kuyaona sasa na tunajivunia kuwa naye.

Inatia moyo na inaonyesha namna gani muziki wa asili unapendwa. Vionjo vya Kiafrika ndani ya muziki vina upekee ambao hauwezi kupatikana popote pale, lakini utandawazi umetulazimisha kuuchukulia poa muziki wa Kiafrika na kushabikia aina nyingine za muziki kutoka ughaibuni ambao nao kwa sasa wana sampo midundo yetu.

Uzalendo ni muhimu wakati huu, tushirikiane kumpigia kura Msafiri kwa njia ya kuingia kwenye tovuti hiyo (kwa wale wenye simu za kisasa) ili tuongeze idadi ya wasanii waliochukua tuzo za kimataifa.

Tumezoea kuwaona wasanii wale wale kina Ali Kiba, Diamond Platnumz, Vanessa Mdee, Ray Vanny na wengine wengi wa Bongo Fleva, lakini kiu yangu kubwa ni kuona muziki wa asili nao unageuka na kuwa dili, unaingia kwenye mfumo wa kibiashara na wasanii wake wale sahani moja kwenye dili za wanamuziki wengine pendwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.