Madiwani sita mbaroni

Mtanzania - - Kanda - Na HARRIETH MANDARI

JESHI la Polisi Mkoa wa Geita limewakamata madiwani sita kwa tuhuma za kuhusika kwenye vurugu za ukataji wa bomba linalopeleka maji katika migodi ya kampuni ya uchimbaji madini ya Geita Gold (GGM).

Pia madiwani hao wanatuhumiwa kuziba barabara zinazoingia ndani ya mgodi huo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema zoezi la kuwatafuta wengine kwa ajili ya uchunguzi linaendelea na kila aliyeshiriki vurugu hiyo atatiwa mbaroni.

“Ningeomba jamii ielewe kuwa madiwani hao na wananchi walioshiriki kutenda makosa hayo ni watuhumiwa kama walivyo watuhumiwa wengine, kwani hawakuchaguliwa na wananchi ili wawe juu ya sheria, bali wahakikishe kuwa sheria hizo ndogo katika kata zao hazivunjwi,” alisema.

Akaongeza kuwa, ameshangazwa kwa vitendo vilivyofanywa na watendaji hao, ambao wao ndiyo walioshiriki kuziunda sheria ndogo hizo na kuzipitisha, lakini wameamua kuzivunja kwa kudhamiria.

Alikataa kutaja majina ya waliokamatwa kwa madai kuwa itaharibu upelelezi unaoendelea, hata hivyo, alisema miongoni mwa watuhumiwa hao sita, watano ni madiwani na mmoja ni Katibu Mwenezi wa UVCCM.

Pia amewaonya madiwani ambao wamekimbilia mafichoni nje ya mkoa huo kwa kusema kwamba wasijidanganye kwa sababu sheria ya kuwakamata haina ukomo wa muda.

“Wakae wakijua kuwa kukimbia au kujificha siyo ufumbuzi na kosa la jinai na sheria ya makosa yao haina ukomo, hata wakikimbilia Afrika Kusini,” alisema.

Sakata la mgogoro kati ya Halmashauri za Mkoa wa Geita na Kampuni ya GGM limechukua sura mpya baada ya halmashauri ya mkoa huo kudai malimbikizo ya kodi ya huduma kiasi cha dola za Kimarekani 12,645,345.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.