KUTOKA KWA MHARIRI Aslay anaweza kupenya katikati ya bifu la Diamond, Kiba

Mtanzania - - Swaggaz -

SOKO la muziki wa Bongo Fleva linazidi kukua siku hadi siku. Wanamuziki wamebadili maisha yao kupitia vipaji vyao. Kiujumla Bongo Fleva imefanikiwa kukaa kileleni, kifua mbele ya Bongo Dansi na Bongo Muvi.

Miaka kadhaa nyuma mambo yalikuwa tofauti. Ilikuwa Bongo Fleva, Bongo Dansi kisha Bongo Muvi – baadaye ikawa Bongo Fleva, Bongo Dansi kisha Bongo Muvi kabla ya Bongo Muvi kushikilia usukanu kwa muda mrefu ikifuatiwa na Bongo Dansi kisha Bongo Fleva.

Kwa sasa mbabe ni Bongo Fleva, Bongo Muvi kisha Bongo Dansi. Hata hivyo ushindani kati ya tasnia zote hizo ni kama haupo au umeachana mbali. Bongo Dansi na Bongo Muvi wamelala.

Wapo wasanii au bendi unazoweza kusema bado zinatamba pamoja na hali ngumu ya muziki huo kwa sasa. Christian Bella ni miongoni mwa wasanii wachache wanaoendelea kuupa uhai Bongo Dansi kutoka na juhudi zake binafsi.

Hapo nyuma Yamoto Band walikuja na kitu cha tofauti. Mtindo wao wa nusu Bongo Fleva, nusu Bongo Dansi ulileta ladha tofauti na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuteka soko. Hivi sasa wasanii waliokuwa wakiunda kundi hilo wamesambaratika.

Kinara wa bendi hiyo Aslay ameanza kuonyesha makali yake baada ya kuanza kutoa nyimbo zake kama msanii wa kujitegemea. Nyimbo zote alizotoa, hakuna hata moja aliyokosea. Ni ngoma zenye makali ya aina yake.

Ukisikiliza kazi zake kama Baby, Angekuona na Mhudumu unaweza kuelewa ninachosema. Ni pini zenye mashiko na zilizokubalika sana kwa mashabiki. Pengine kama siyo hizi kelele za Ali Kiba na Diamond na ushindani wao wa kiki na bifu, Aslay angetusua zaidi.

Hakuna shaka kwamba wasanii Diamond na Kiba ndiyo wapo kileleni kwenye Bongo Fleva hivi sasa, lakini staili yao ya bifu ambayo imefikia kiwango cha kutokuwa na ustaarabu, inaweza kuwa kete ya ushindi kwa Aslay.

Aslay asiingie kwenye mkenge wa bifu, kiki wala ushindani wa team, ajikite katika kufanya kazi nzuri, promo ya kutosha na kupiga shoo za maana. Hili ataweza kufanikiwa kama atakuwa na menejimenti nzuri.

Katika hilo anapaswa kujipanga, lakini siyo kwa kumzuia Aslay kupita katikati ya Kiba na Diamond, wao waendelee na bifu lao, yeye atusue kimuziki.

Uzuri ni kwamba historia ya Aslay inajipambanua wazi namna alivyo msanii mkali. Tangu mwaka 2011 (miaka sita sasa) alipoachia Naenda Kusema akiwa mtoto mdogo, ameendelea kuonyesha uwezo wake mpaka sasa.

Ni zamu yake kuwaweka pembeni Kiba na Diamond na kuipaisha Bongo Fleva yenye ushindani wa kweli. Kazi ni kwako Aslay.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.