Kauli ya JK kuntu, demokrasia iheshimike

Mtanzania - - Jicho Pevu - Na TOBIAS NSUNGWE

MWALIMU Julius Nyerere anakumbukwa kwa mambo mengi aliyopata kuyafanya ndani na nje ya Taifa letu na kuiacha nchi ikiwa salama salimini.

Hotuba zake nyingi zililenga kuimarisha udugu na mshikamano. Hakuacha kukemea rushwa na kuhimiza utawala bora wenye kuheshimu utu wa mtu.

Katika ulingo wa kisiasa unapolizungumzia jina la Mwalimu Nyerere, ni wazi kuwa jina la Jakaya Kikwete (Rais Mstaafu wa awamu ya nne) halitabaki nyuma, kutokana na historia yake, kwani ametumia karibu maisha yake yote ya ujana kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tangu ahitimu elimu ya Chuo Kikuu mwaka 1975, amekuwa akifanya kazi za CCM katika ngazi mbalimbali hadi kufikia kuwa Rais wa nchi na Mwenyekiti wa chama hicho mwaka 2006.

Kikwete anaijua CCM vizuri sana. Wanasema CCM ina wenyewe, huenda mmoja wa wenyewe ni Kikwete.

Yapo mambo mengi yanayofaa kumkumbuka Rais huyo mstaafu ndani ya Chama na Taifa kwa ujumla.

Tangu akiwa madarakani Kikwete alisisitiza amani kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Pia, alisisitiza umuhimu wa wanaCCM kuwasikiliza wapinzani, jambo ambalo baadhi ya wana-CCM walishindwa kumwelewa.

Kikwete alisaidia kuwaondoa ‘ushamba’ baadhi ya makada wa CCM waliokuwa wakidhani kwamba vyama vingine ni maadui. Kikwete aliacha pia taswira nzuri kwa vizazi vijavyo katika chama hicho, kwamba mwanachama mmoja hawezi kuwa mkuu kuliko chama eti kwa sababu tu ana fedha za kuhonga watu.

Aliimarisha uhusiano na vyama vingine rafiki kama Swapo cha Namibia, ANC cha Afrika Kusini, Chama cha Kikomunisti (CCP) cha China na kile cha Vietnam. Kikwete pia alisisitiza dhana ya chama kujitegemea kiuchumi. Hivi sasa CCM ina kituo chake cha mikutano mjini Dodoma.

Chini ya Kikwete, wanachama na wapenzi wa CCM walihamasishwa kuchangia chama hicho bila kutegemea hisani yoyote kwa siku za baadaye.

Amefanya mambo mengi, nadhani atakumbukwa zaidi kwa mambo makuu mawili. Kwanza kuishawishi CCM ikubali kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.

Mchakato huo ulioanza mwaka 2011, ulipongezwa na wadau mbalimbali, hasa vyama vya siasa, hususan upinzani.

Bado hatujapata Katiba mpya, lakini walau Kikwete alianzisha mwendo. Jambo la pili ni pale alipowabana watu aliowaona kuwa hawafai kupitishwa kugombea urais.

Kikwete aliondoka huku akiiacha nchi ikiwa salama. Pia amemkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa CCM chama kikiwa salama, licha ya kuwapo kwa makundi ambayo kimsingi huwa hayaondoleki.

Mwenyekiti wa sasa bado ana kibarua kigumu cha kudhibiti vitendo vya rushwa vilivyozoeleka ndani ya chama hicho, hasa katika kipindi cha uchaguzi ndani ya Chama.

Kikwete amestaafu mikikimikiki ya siasa za ndani, anatumia muda wake kutekeleza majukumu mengine ya kimataifa.

Majukumu ya kimataifa ni pamoja na kuhudhuria kwenye Kongamano la Uongozi Afrika mwaka 2017, lililofanyika nchini Afrika Kusini, Agosti mwaka huu.

Katika kongamano hilo la siku mbili alitoa kauli maridhawa ambayo ilizua mjadala nchini na hata nje ya Taifa letu.

Kikwete alitumia jukwaa hilo kuvionya vyama tawala barani Afrika kuacha kuvichukulia vyama vya upinzani kama maadui, bali wavione vyama hivyo kama washindani wao.

Kauli hiyo imesifiwa na viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani ndani na nje ya nchi. Kiongozi wa Chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini (DA), Mmusi Maimane, amesema Kikwete alikuwa ameibua hoja ya umuhimu wa upinzani Afrika kama kazi ya utawala bora.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, amemsifu Kikwete kwa kuwa mvumilivu kwa upinzani wakati wa utawala wake na kwamba alichokisema nchini Afrika Kusini alikuwa akimaanisha.

Katika hoja yake, Kikwete pia aliwataka wabunge wanaotoka vyama tawala kuwa na ujasiri wa kuihoji Serikali pale wanapoona mambo hayaendi vizuri. Lazima wabunge wote kwa umoja wao wasimame imara kuhakikisha mambo yanakwenda kwa mujibu wa matarajio ya wananchi.

Kauli ya Kikwete inakuja wakati bado makada wa vyama tawala Afrika wakiwa bado na ‘ushamba’ wa kuwaona wanachama wa vyama vya upinzani kuwa ni maadui.

Ushamba huo umeonekana kupungua nchini Ghana na Botswana, hata hivyo haujafutika nchini Zimbabwe, Afrika Kusini, Kenya, Burundi, Rwanda, Zambia na hata Tanzania.

Hata alipokwenda bungeni kushuhudia mkewe, Mama Salma Kikwete akila kiapo cha ubunge, Rais huyo mstaafu alishangiliwa na wabunge wote, huku wale wa upinzani wakidai kumkumbuka!

Sauti za wabunge wa upinzani kumshangilia Kikwete zilituma ujumbe kwamba, baada ya yeye kutoka madarakani Novemba 5, mwaka 2015, mazingira ya kufanya kazi kwa vyama vikuu vya upinzani, yaani Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi yamekuwa magumu mno.

Kilio cha wapinzani na wanaharakati kila kona nchini ni kwamba utawala wa sasa unaminya demokrasia. Kwanini? Kwa kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara ya siasa. Malalamiko mengine ni wabunge wa upinzani kuingia kwenye misukosuko na polisi kila wakati. Inaelekea utawala wa sasa unakosa uvumilivu wa kuhimili kukosolewa, jambo ambalo halileti afya kwa ujenzi wa demokrasia nchini.

Akizungumzia madai ya upinzani kudai kufanya maandamano, Rais Magufuli aliwahi kunukuliwa akisema kuwa yeye atakuwa na msimamo ‘tofauti sana’ juu ya ushirikiano na wapinzani. Ndio maana tukaona maandamano yakizuiwa. Karibu nusu ya Watanzania ni wapenzi au wanachama wa vyama vya upinzani. Hivyo lazima sauti yao isikike kupitia wawakilishi wao.

CCM haijawahi kuwa na Serikali ya malaika. Lazima itafanya makosa. Nchi inahitaji upinzani kuikosoa Serikali pale utawala unapokosea. Ni muhimu utawala wa sasa uweke mazingira rafiki ya kuwawezesha wapinzani kuikosoa kwa nidhamu Serikali iliyopo madarakani. Tunawahitaji wapinzani kusemea wananchi pale Serikali inapojichanganya.

Tunahitaji sauti za vyama vya upinzani kama Chadema kupiga kelele ili kukomesha tabia ya Serikali kuwaachia watu wajenge katika maeneo yanayodaiwa kukatazwa na baada ya muda kuwabomolea! Siasa isipewe nafasi linapokuja suala nyeti kwa wananchi kama makazi.

Sauti ya Kikwete toka ardhi ya Mzee Madiba isaidie kuwatoa ‘ushamba’ baadhi ya viongozi wa Serikali ya CCM na hivyo waondoe vikwazo vyote vinavyowazuia wapinzani kufanya kazi zao. Idadi kubwa ya vikwazo hivyo imepitwa na wakati.

Jakaya Kikwete

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.