Uhuru wa Korea Kaskazini umekuwa kero?

Mtanzania - - Jicho Pevu -

NINAPENDA kushirikiana na wasomaji wa gazeti hili la MTANZANIA kutafakari suala la uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na mataifa ya nje, pamoja na Korea Kaskazini na mataifa mengine.

Napenda tuongelee kwa ufupi juu ya sekeseke linaloendelea kati ya Korea Kaskazini dhidi ya dola la Marekani na washirika wake, Japan, Korea Kusini na wengine kama Uingereza, Ufaransa na kadhalika.

Kwanza kabla sijaeleza kuhusu Korea Kaskazini, nawakumbusha wasomaji namna dola ya Libya ilivyoanguka. Ni ukweli usiopingika kuwa, dola ya Libya iliangushwa mara baada ya Jemedari Muammar Gaddafi kukubali kufifisha uwekezaji wake katika silaha za kujilinda dhidi ya jamii ya kimataifa.

Wengi wanamtazama Kanali Gaddafi kama Jemedari aliyefanya yote, lakini akakubali kudanganywa kuwa ulinzi wa watu wake siyo jukumu lake. Sote tunakubaliana kuwa yeye atabaki kuwa mtu muhimu na mwenye nguvu aliyetokea bara la Afrika.

Kiuhalisia, dola ya Libya ilianguka Desemba mwaka 2003, pale Gaddafi aliporuhusu wakaguzi kutoka Marekani na Ulaya kuingia nchini mwake na kukagua silaha zake, kisha kumtaka asiendelee kuzalisha silaha walizoziita za maangamizi.

Kilichotokea mwaka 2011 ni sawa na kuvunja biskuti tu. Dola ya Libya imeanguka. Utajiri wote wa Libya umekwisha, nchi iliyokuwa neema kwa bara la Afrika imekuwa laana. Raia wanauana na kuuzana, nchi moja ina serikali zaidi ya moja. Mbaya zaidi, Marekani na Ulaya wanachekelea. Kujali kwao kumekwisha. Hawana muda tena na hatima ya Libya.

Turudi kwenye mkasa wa sasa wa North Korea. Taifa la Korea Kaskazini linaendelea kuwa Taifa la pekee lililojitoa kuhakikisha kuwa usalama wa watu wake unakuwa kipaumbele cha kwanza.

Ni mfano wa kuigwa, hasa na taifa lenye rasilimali nyingi na adimu kama Tanzania. Jana nilisoma taarifa ya Waziri wetu wa Mashauri ya nje, Dk. Augustine Mahiga, akiwa anajitetea baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kusema kuwa, Tanzania tumekuwa na uhusiano na Korea Kaskazini.

Nachelea kusema huu ni utumwa. Utumwa wa kuchaguliwa marafiki. Marehemu Nelson Mandela aliichukia Israel kwa sababu iliungana na makaburu waliotesa watu weusi huko Afrika Kusini.

Mandela alipoulizwa akasema kuwa, moja ya makosa Marekani na washirika wao wanayofanya ni kudhani kuwa maadui zao ni lazima wawe maadui zetu. Ila kwa nchi kama yetu hilo haliepukiki. Utumwa wa misaada tunayopokea. Tukaze buti. Hakuna sababu ya kujitetea kuwa tunawachukia Korea Kaskazini ili tuwapendeze wakubwa wa Marekani, ilhali tunajua ukweli kuwa Korea Kaskazini wanalinda watu wao. Ni lazima nasi tuwe na mipango ya kuimarisha ulinzi.

Nihitimishe kwa kuipongeza Korea Kaskazini kwa juhudi wanayofanya kuhakikisha kuwa wanakuwa dola huru na inayoheshimika ulimwenguni. Wanatufundisha kuwa na akili zetu timamu bila kushikiliwa. Sisi ni Taifa huru na katika dunia hii ya kuuana ni lazima tuwe na msuli wa kuthibitisha uhuru wetu. Ni lazima kuulinda. Hivi uhuru wa Korea Kaskazini umekuwa kero kiasi hicho?

0752 885 610

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.