Ndanda wamwita Malale Hamsini aokoe jahazi

Mtanzania - - Michezo - Na MOHAMED KASSARA

UONGOZI wa Ndanda FC umeweka mikakati ya kuhakikisha wanamrejesha kocha wao wa zamani, Hamsini Malale, ili abebe jukumu la kukinoa kikosi hicho.

Malale aliwahi kuinoa Ndanda, yenye maskani yake mjini Mjini Mtwara, kabla ya kutimkia Ruvu Shooting na baadaye kujiunga na KMKM za Zanzibar.

Klabu hiyo hivi karibuni ilimfungashia virago kocha wake mkuu Mmalawi, Ramadhani Nsanzurwino, aliyeiongoza timu hiyo katika michezo miwili pekee ya msimu huu na jukumu la kuiongoza kupewa msaidizi wake, Mussa Mbaya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa Ndanda, Suleiman Kachele, alisema wako katika mazungumzo na kocha huyo ili achukue jukumu la kukinoa kikosi chao kama kocha mkuu.

Alisema mazungumzo yanaendelea vizuri na pale watakapokubaliana kocha huyo atarejea kukinoa kikosi cha timu hiyo kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

“Ni kweli tupo katika mazungumzo na Malale ili arejee kukinoa kikosi chetu, tumefanya hivyo kutokana na kuthamini mchango wake, kwani msimu uliopita aliiweka timu yetu katika nafasi nzuri,” alisema Kachele.

Malale alipotafutwa ili azungumzie msimamo wake, alisema anazo taarifa hizo za kuhitajika tena kukinoa timu hiyo, lakini atakuwa tayari kurejea ikiwa watakubaliana katika suala zima la maslahi yake.

“Kwa sasa niko zangu nyumbani Zanzibar naendelea na kazi yangu KMKM, hivyo kama tutaelewana sina pingamizi, nitarudi kukinoa kikosi cha Ndanda, kwavile sikuondoka kwa ubaya katika timu yao,” alisema Malale.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.