Guardiola: Huyo Mbappe hagusi kwa Messi

Mtanzania - - Michezo -

KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amezisikia tetesi zilizozagaa kuwa staa Kylian Mbappe anakaribia kuufikia ubora wa Lionel Messi, lakini Mhispania huyo amezipuuzia akisema ni upuuzi mtupu.

Guardiola anamjua vizuri Mbappe, kwani msimu uliopita mabao mawili ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 yaliiwezesha Monaco kuitoa Man City kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini pia, Mbappe aliifungia Monaco jumla ya mabao 26 katika mechi 44 na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligue 1 na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbali na yote hayo, bado Guardiola anaamini makali aliyonayo ‘dogo’ huyo kwa sasa hayawezi kumfikia Messi, aliyewahi kufanya naye kazi katika klabu ya Barcelona. “Hakuna anayeweza kukaa meza moja na Messi,” alisema Guardiola.

“Labda Mbappe ni mchezaji mzuri, atakuwa moto zaidi, nina uhakika. Lakini kufananisha na kile ambacho Messi amekifanya kwa miaka 10 au 12, au Cristiano (Ronaldo), tunapaswa kusubiri.

“Nafikiri Messi ana mechi 60 au 70 kwa kila msimu, mechi kubwa, na mara nyingi amekuwa akifunga na kutoa ‘asisti’, hajaumia, anacheza mara tatu kwa wiki.”

Akiizungumzia Man City katika mbio za ubingwa msimu huu, Guardiola alisema anataka kumaliza utegemezi uliopo kwenye idara ya mabao, ambapo mzigo mkubwa wa kuzitikisa nyavu upo kwa Sergio Aguero na Gabriel Jesus.

“Sitaki kuwapa mzigo mkubwa Sergio au Gabriel. Timu ni nzuri inapokuwa na uwezo wa kufunga mabao,” alisema kocha huyo, aliyewahi pia kuinoa Bayern Munich.

Arsene Wenger

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.