Wakimbizi raia wa Burundi wauawa DRC

Mtanzania - - Jicho Pevu -

TARKIBANI wakimbizi 18 wameripotiwa kuuawa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Idadi hiyo ni ya awali iliyotolewa, ingawa huenda ikaongezeka kutokana na kukosekana idadi kamili ya watu walioshambuliwa.

Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi wa Congo wamewapiga risasi na kuwaua wakimbizi 18 wa Burundi, kufuatia mapigano yaliyozuka katika eneo la Kamanyola, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kwa mujibu wa maofisa wa eneo hilo katika Mkoa wa Kivu Kusini waliotoa idadi hiyo ya awali ambayo huenda ikawa zaidi, wamesema kwamba, huenda zaidi ya wakimbizi 30 wameuawa na wasiopungua 100 wamejeruhiwa.

Ofisa mmoja kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, Josue Boji, amesema wanajeshi walijaribu kuwatawanya wakimbizi kwa kufyatua risasi hewani, lakini walizidiwa nguvu baada ya kundi kubwa la wakimbizi kuvamia gereza linalosimamiwa na shirika la ujasusi wa ndani, wakitaka raia wanne wa Burundi wanaoshikiliwa katika gereza hilo waachiwe huru.

Inatajwa kwamba, idadi ya awali inaweza ikaongezeka kutokana na wakimbizi hao kuzitwaa baadhi ya maiti za watu wengine waliouawa na kuzipeleka katika kambi ya Umoja wa Mataifa inayosimamiwa na wanajeshi wa Pakistan katika eneo la Kamanyola.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.