TAFAKURI YANGU

‘Tunaiweka rehani amani yetu kwa kisichojulikana’

Mtanzania - - Jicho Pevu -

HAIWEZEKANI kubadilisha asili ya mtiririko wa matukio, isipokuwa kwa namna mbadala kuhusiana na kadhia.

Inawezekana usinielewe, lakini zama katika tafakuri utaelewa kuwa leo unaposoma safu hii isingewezekana kujiri kama majuzi, juzi na jana hazikujiri, ikimaanisha kuwa kesho, keshokutwa na mtondogoo hazitajiri ila lazima zitatimia.

Wakati hauzuiliki, ingawa una vipimo tofauti vya majira na nyakati, kwa mujibu wa kalenda tofauti duniani, ukiachilia mbali mfumo wa ujumla tunaoutumia kuhesabu siku.

Hata matukio mabaya yana chanzo cha mtiririko, hata kama hayahusiani moja kwa moja, anayetenda uhalifu anachachusha na kuumua uhalifu wa wengine wanaoona upenyo wa fursa ya kutimiza mabaya yao.

Kwa lugha nyepesi naweza kufananisha na kuoka mkate kwamba, bila amira ya kuuchachusha na kuumua kwa moto mekoni hautaiva.

Jambo ninalolilenga si jepesi kama kuoka mkate na kuutafuna.

Tulizoea kuitwa ‘kisiwa cha amani’ kwa kuwa majirani zetu wote wanaotuzunguka wamegubikwa mitikisiko ya hamkani za mapigano, uhalifu, hata misigano inayowatikisa, sasa taratibu tunageuka uwanda wa vurumai zinazoongezeka kadiri siku zinavyokwenda.

Lilipotokea tukio baya kabisa katika historia ya siasa hapa nchini juma moja na ushei lililopita, nilitarajia mwitiko uliofuata kutoka makundi mbalimbali kuhusu anayehusika, lakini hamkani zenye mashiko ya kiitikadi, hususan mtazamo wa mrengo wa kumnyamazisha Tundu Lissu, upande mwingine ukaibuka na msamiati mpya wa ‘wasiojulikana’, wanaofanya mambo kwa dhamira isiyojulikana.

Ushabiki ukatamalaki na kukinzana na weledi wa kipelelezi na mitandao ya kijamii kugubikwa mijadala isiyofurahisha iliyojaa kedi, kebehi, matusi na mengine mengi katika muda mfupi sana tangu kutokea kwa tukio husika.

Kilichosababisha nitarajie hali hiyo ni kutokana na hulka tuliyonayo ya kushughulikia matukio kama hayo, ikiwamo kukosa subira, kwani tunapenda sana kukimbilia kulaumu na hatutoi nafasi kwa weledi kushughulika na kutoa majibu.

Ninagubikwa na hoja nyingi zilizokosa majibu kwenye ‘Tafakuri Yangu’ na msingi wake ni orodha ya matukio machache ninayoyakumbuka, mengine si ya miaka ya hivi karibuni, lakini bado yamejigubika utata wa kufahamika kiini chake.

Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na kuuawa kwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Nicas Mahinda, kukatwa mapanga Dk Sengondo Mvungi na kusababisha kifo, kuvurumishwa bomu kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti mkoani Arusha, kupigwa risasi kwa Askofu visiwani Zanzibar, mauaji ya watendaji wa kiserikali wa ngazi za vijiji wilayani Kibiti na Mkuranga, kuvurumishwa mabomu ya kienyeji kwenye ofisi ya wanasheria wa IMMMA, kupigwa risasi kwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba na matukio mengine ambayo sikuyaorodhesha unayoweza kuyakumbuka.

Kinachonisumbua ni kukosekana kwa majibu yanayoridhisha baada ya kuchunguzwa na kufanyiwa kazi matukio hayo, hususan yanavyohusishwa kimakosa na mashiko ya kisiasa bila upembuzi yakini, hilo likijiakisi kwa kila upande kwa kuwa moja kati ya nisilokubaliana nalo ni dhana kwamba mamlaka inaweza kufanya tukio kama lililomfika Lissu kwa utashi na uamuzi wa kiujumla. Ingawa pia siwezi kukataa hisia kwamba huenda kuna watu kwenye ngazi mbalimbali ambao kwa utashi wao binafsi wanaweza kutamani kufanya hivyo.

Hapo ndipo weledi unapopaswa kutamalaki kwa kuachiwa nafasi na walinzi wa usalama, likiwamo Jeshi la Polisi ndio wanaopaswa kutupa majibu yenye uhakika. Lakini ili turidhike tuwekwe wazi kijulikane hicho kisichojulikana ili yeyote mwingine anayedhamiria kufanya kama walivyofanya wahalifu wenzake, afahamu kuwa mkono wa sheria utamkumba na kumdhibiti bila kujali ni nani, yuko wapi na kwenye nafasi gani.

Kupoteza mwelekeo kwa maoni ya waliohemkwa mitandaoni ni kujivisha hulka ya vita vya panzi na kunguru, wahalifu wanaohanikiza yanayotokea lazima watafurahi kupata nafasi ya kuhanikiza maovu zaidi.

Kupima kwa mtazamo tenge taarifa ipi ya kuchukulia hatua na ipi ya kuiacha kutokana na ilipotamkwa nako kunazidisha ugumu wa kupata ufumbuzi.

Kama waliotekeleza shambulizi dhidi ya Lissu waliwahi kutajwa pia na wabunge wengine, tena wakitaja namba zile zile za gari wanayotumia pamoja na wajihi wao, kwa nini hatua madhubuti hazikuchukuliwa? Kwamba sasa makada wa chama anachotoka Lissu wakiongea kwenye mikutano na waandishi wa habari ionekane kuwa chanzo cha taarifa hitajika kulikabili jambo hilo, inanitia mashaka, nadhani hata kama si taaluma yangu, taarifa zilizotolewa awali kwa kufuata utaratibu zingeangazia mahali pazuri pa kuanzia.

Wenye mihemko kama mlisahau niliwahi kubainisha kwamba, kuachiwa kwa mtiririko wa matukio mabaya yaliyokosa majibu hata yanapofanikiwa kudhibitiwa, kutasababisha wabaya wetu kusimama katikati yetu na kutumia tofauti zetu za mitazamo kutugonganisha, ambapo kwa asilimia fulani wamefanikiwa.

Tusipokuwa na amani hatutaweza kutafuta maendeleo, nchi yetu inapaswa kurudia kuwa kisiwa cha amani, si kisiwa cha mitutu ya wasiojulikana!

Waumini wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, wakikimbia baada ya kutokea shambulizi la bomu mkoani Arusha.

Marehemu Dk. Sengodo Mvungi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.