Mihemko ya kisiasa kumng’oa Jaji Maraga?

Mtanzania - - Jicho Pevu - MARKUS MPANGALA Na MITANDAO

HAWAMTAKI Jaji Mkuu David Maraga wala Msajili wa Mahakama Anne Amadi. Ni kauli rahisi ambayo inafafanua hoja binafsi inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni na wabunge wa Chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta, ambacho kipo pia kwenye kampeni za urais katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika Oktoba 17, mwaka huu.

Wabunge wa chama cha Jubilee wamechukua hatua hiyo na kusisitiza kwamba, watawasilisha hoja binafsi za kumwondoa Jaji Mkuu Maraga na Msajili wa Mahakama Amadi, baada ya kukamilika mafunzo kwa wabunge wenzao wapya kabla ya kuanza rasmi shughuli za Bunge.

Kwa mujibu wa Chama cha Mahakimu na Majaji (KMJA), kimesema imebainika pia hoja hiyo inatokana na mivutano ya kisiasa na kisheria dhidi ya Jaji Mkuu, David Maraga, kwa lengo la kumwondoa katika nafasi yake limechochewa na uamuzi wa kufuta matokeo ya urais ya Agosti 8, mwaka huu.

Taarifa zinasema kuwa, hatua ya wabunge hao kulitumia Bunge inatokana na kushindwa ‘kupitia’ Tume ya Kimahakama na Huduma. Katibu Mkuu wa KMJA, Bryan Khaemba, amesema mpango wa chama cha Jubilee kumwondoa Jaji Mkuu hautafika kokote, kwasababu Mahakama ni chombo huru.

“Tunafahamu idadi ya wabunge wanaoshinikiza kuondolewa Jaji Mkuu na Msajili wa Mahakama kutokana na hukumu iliyotolewa karibuni ya kufuta matokea ya urais na kuagiza uchaguzi urudiwe. Napenda kuwakumbusha kuwa, hatua inayochukuliwa dhidi ya Jaji Maraga inabeba maana halisi ya utawala wa kisheria, na pia tafsiri ya wazi kuwa nchi inatawaliwa na sheria au kundi la watu,” alisema Khaemba. JUBILEE WAKANA Katika hatua, nyingine chama cha Jubilee kimekataa kujihusisha na mpango wa kumwondoa Jaji Mkuu huyo na kusema hakifahamu chochote juu ya hatua hiyo iliyotangazwa na Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Raphael Tuju, ameviambia vyombo habari kuwa chama cha Jubilee hakiwajibiki kwa hatua iliyotangazwa kwasababu hakikushirikishwa. Tuju amesema Ngunjiri Wambugu amewasilisha hoja za kumng’oa Jaji Mkuu yeye binafsi na si uamuzi wa chama.

“Nimesikia kupitia vyombo vya habari kuhusu hilo, lakini chama cha Jubilee hakikushirikishwa kwenye mpango huo. Huo ni mpango wa wabunge wenyewe kwa nafasi yao,” alisema Tuju. HOJA ZA NGUNJIRI WAMBUGU Huyu ni Mbunge wa Nyeri Mjini kupitia chama cha Jubilee. Ndiye mwandaaji wa hoja binafsi ya kumwondoa Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu, Maraga. Wambugu anamtuhumu Jaji Maraga ni kiini cha Majaji wa Mahakama ya rufani kutoa uamuzi kwa maslahi ya Raila Odinga.

Mbunge huyo anadai kuwa, Maraga alitoa shinikizo kwa majaji hao katika uamuzi wao. Aidha, ametoa orodha ya watu waliomsaidia Jaji Maraga kuchukua uamuzi wa kufuta matokeo ya urais ambao hawakupendezwa na ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Katika hoja binafsi aliyoandaa yenye jumla ya kurasa 14, mbunge huyo anamtuhumu Maraga kushirikiana na asasi moja ya kiraia yenye ushirikiano na muungano wa vyama vya upinzani, Nasa pamoja na mgombea wao, Raila Odinga.

Profesa wa Sheria, Makau Mutua, ambaye ni mkosoaji wa chama cha Jubilee, ametajwa kumsaidia Jaji Maraga pamoja na Mwanaharakati Maina Kiai na asasi nyingine za kiraia. Katika orodha yake ameyataja mashirika ya kimataifa ambayo yanatoa msaada wa hali na mali kumwezesha Odinga kumshawishi Maraga atoe hukumu ya upendeleo.

Majaji wanne kati ya sita walikubaliana kwa kauli moja, uchaguzi wa urais urudiwe. Majaji hao ni Jaji Mkuu David Maraga, Jaji Smokin Wanjala, Jaji Isaac Leonaola na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu. Majaji wawili waliopinga kurudia uchaguzi huo ni Jaji Njoki Ndung’u na Jaji JB Ojwang, wakati jaji Mohammed Ibrahim hakuwapo mahakamani. WANAOTUHUMIWA Watu waliotuhumiwa orodha yao imetajwa na Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu kuwa ilishiriki kushinikiza kufutwa matokeo ya urais.

Profesa Makau Mutua: Mshauri wa Bodi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria (IDLO). Shirika ambalo husaidia katika programu za maendeleo katika sekta ya sheria.

Mburugu Gikunda: Zamani alifanya kazi katika taasisi ya Media Focus on Africa. Anadaiwa ndiye alifanya kazi kubwa kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Fleur Van Dissel: Huyu ni mtengenezaji wa makala ya Odinga (Documentary) ambaye ni raia wa Uholanzi. Alifanya kazi zake kwa ukaribu na Mburugu Gikunda.

Zeph Aura: Msiri mkubwa wa Raila Odinga. Amewahi kutafuta nafasi ya kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), lakini akashindwa na Ezra Chiloba. Kwa sasa anafanya kazi na Shirika la USAID la Marekani.

Otieno Odek: Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Kisheria. Duncan Okello: Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kitaifa kuhusu Utekelezaji Sheria. Wambugu anadai, iliundwa kinyume cha sheria.

Atieno Odhiambo: Karani wa zamani Sheria wa Jaji Mkuu ambaye humshauri kuhusu kesi za Mahakama ya Juu.

Ivan Marovic: Mwanachama wa Shirika la Wakazi wa Siberia Otpor.

Gladwell Otieno, Harun Ndubi, Betty Murungi, George Kegoro, Ndungu Wainaina na Ben Sihanya: Wanachama wa Vuguvugu la mashirika ya haki Kenya.

Steve Ouma: Naibu Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Tume ya Haki za Binadamu.

Linda Musumba: Mwanachama wa Bodi ya Kituo Cha Sheria.

Moses Owuor: Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Kenya.

Collins Odote: Mjumbe wa Kamati ya Mahakama kuhusu Ushauri wa sheria ya Uchaguzi.

Odhiambo Makoloo: Msimamizi Mkuu wa Taasisi ya Ford.

Violet Mavisi: Kamishna wa zamani wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR). KUONDOLEWA JAJI MKUU Hoja binafsi ya kumwondoa Jaji Mkuu inapaswa kuwasilishwa kwa Spika wa Bunge. Naye Spika wa Bunge ataipitia hoja hiyo kujiridhisha kama imekidhi vigezo, kisha atawasilisha bungeni kwaajili ya kukusanya sahihi za wabunge angalau theluthi mbili, sawa na wabunge 349.

Nayo Ofisi ya Spika itakuwa na wajibu mwingine wa kuhakiki sahihi zote za wabunge kama wamefikia vigezo vya kisheria vinavyohitajika, kabla ya kushauriana na idara ya sheria ya Bunge kuandaa hoja hiyo na kuipeleka katika Kamati ya shughuli za Bunge ili kuipangia tarehe ya kusomwa na kujadiliwa.

Jaji Mkuu David Maraga

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.