Ameniacha kisa sina fedha

Mtanzania - - Rose -

H abari Anti, MIMI ni kijana nipo Tanga, nipo katika uhusiano na mpenzi wangu kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa.

Mwanzoni tulikuwa tukiishi kwa amani na upendo, japokuwa tulikuwa na vikwazo mbalimbali vya kawaida ambavyo havikuweza kusababisha kuachana.

Kwa sasa mpenzi wangu amebadilika sana, nahisi ameanza uhusiano na mtu mwingine, sikukaa kimya, niliamua kuchunguza nikagundua ni kweli.

Kutokana na hali hiyo nililazimika kumuuliza, jibu alilonipa ni kwamba anatafuta maslahi ya kifedha pamoja na kwamba na mimi ananipenda. Nifanyeje wakati bado nampenda na namuhuduma kila kitu.

JIBU

Pole kwa mtihani uliokukuta, kwanza unapaswa kujua hakuna penzi la kweli linalostawishwa na fedha, kama unampa mpenzi wako fedha siyo ishara ya kumridhisha, vipo vitu ambavyo vinamfanya mtu aridhike katika mapenzi kutoka ndani ya moyo wake.

Mtu ambaye anakupenda kutoka moyoni anaweza kukubali kuishi na wewe katika hali yoyote bila kujali kipato chako wala matatizo yako,lazima utambue mapenzi ni hisia zinazofanana na kuwaunganisha watu wawili.

Lakini mbali na mapenzi tu ya kawaida, pia wapo wanawake ambao wanaendekeza zaidi tamaa kuliko kuangalia moyo wake unataka nini.

Tambua kuwa hakuna mapenzi ya watu kukubaliana, hasa hili la kutafuta maslahi kwa kuanzisha uhusiano mwingine, hapo ni wazi kuwa nafasi yako katika moyo wake haipo.

Kama ni kweli maslahi yamemfanya akusaliti, ni wazi kuwa hakuwa na penzi la kweli, badala yake alipenda fedha zako tu.

Nakushauri kaa na mpenzi wako umbane akueleze kinachomsibu mbali na hilo, ikiwezekana mtishie kumuacha, ukimuona hajashtuka utambue kuwa mtu huyo hakutaki lakini anaogopa kukwambia kweli.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.