Mbunge CCM amfuata Lissu

Bavicha wasema maombi yako palepale

Mtanzania - - Mbele - Na AGATHA CHARLES –DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), amefika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kumjulia hali Tundu Lissu aliyelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) tangu Septemba 7, mwaka huu akipatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Nyalandu kupitia akaunti zake, zikiwamo za Facebook na Instagram, jana alisema pamoja na kufika hospitalini hapo mapema, lakini hakuruhusiwa na madaktari kumwona Lissu kwa muda huo.

Nyalandu ambaye ni mbunge wa kwanza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenda kumwona Lissu hospitalini, alisema akiwa bado akisubiri ruhusa ya madaktari ili kumwona pia alifanikiwa kutoa pole kwa mke wa Lissu.

“Nimefika Hospitali ya Nairobi mapema leo (jana) kumjulia hali Lissu. Madaktari wanaendelea kumfanyia matibabu, na bado hatujaruhusiwa kumuona. Kwa niaba ya wana Singida na Watanzania wote, nimetoa salamu za pole kwa mke wake, na bado nasubiri uwezekano wa kuweza kuonana naye usiku wa leo (jana) endapo madaktari wataruhusu,” aliandika Nyalandu.

Katika andiko hilo ambalo Nyalandu aliambatanisha picha aliyopiga akiwa hospitalini hapo na mdogo wake Peter Nyalandu, aliwataka Watanzania kuendelea kumwombea Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki ili Mungu amponye katika nyakati hizi za kujaribiwa kwake.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), aliposti picha katika ukurasa wake wa Facebook akiwa na Nyalandu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari wakiwa nje ya eneo la hospitali hiyo.

Katika picha hiyo, aliandika: “Muelekeo ni muhimu kuliko kasi, wengi hawajui waendako, lakini wanakwenda kwa kasi! Ndiyo maana ni bora nchi moja kwenda kwenye muelekeo sahihi kuliko maili moja kwenda kwenye muelekeo usio sahihi.”

MAOMBI YA BAVICHA

Wakati huo huo, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), limesema maombi ya leo kumwombea Lissu yapo palepale.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita, kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari.

Kuhusu mikusanyiko ya maombi hayo kupigwa marufuku na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, katibu huyo alisema kuwa kauli hiyo haikueleweka vyema.

“Tumefuatilia kwa kina kuhusu kauli za Kamanda Mambosasa ambazo zimenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo (jana) ikidhaniwa kuwa amezuia shughuli hiyo ya maombi na tumebaini Mambosasa hakueleweka vyema.

“Kwa sababu aliulizwa swali kuhusu shughuli yetu ya kumuombea Lissu, lakini yeye akatoa majibu kwa kuzungumzia maombi ya maandamano ya watu walioomba kibali cha kuwapokea wabunge wao wakiwa wanatokea Dodoma, ndiyo maana akazungumzia maandamano,” alisema.

Mwita alisema walijiridhisha kuwa taarifa iliyopelekwa kwa Jeshi la Polisi kama sheria inavyoelekeza, haikutaja wala kuzungumzia maandamano bali watu wa dini mbalimbali zilizopo nchini wanaoguswa na tukio la Lissu kukutana kwa maombi.

“Hadi sasa tumezingatia taratibu zote za kisheria ambazo zinatuelekeza kutoa taarifa kwa mamlaka za kiserikali, hususani Jeshi la Polisi. Kwa sababu hadi sasa jeshi hilo halijatuandikia barua ya kutuita ili kujadiliana nao kuhusu kufanikisha shughuli hiyo, tunaamini kuwa hawana pingamizi lolote la kiutaratibu kama ambavyo sheria inaelekeza,” alisema.

Katika taarifa hiyo, Mwita alisisitiza kuwa Bavicha ilifanya kazi ya kuratibu maombi hayo, lakini shughuli hiyo ni ya kiimani, hivyo wamealikwa viongozi wa kiroho ili kuendesha maombi hayo ya kumwombea Lissu.

Aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwenye maombi hayo yatakayofanyika kwenye viwanja vya TP, Sinza Darajani, Dar es Salaam, kuanzia saa nane mchana.

Juzi Mambosasa alinukuliwa akisema: “Hakuna kusanyiko linaloruhusiwa, zipo sehemu maalumu za kufanya maombi ambazo hazizuiwi kama vile makanisani na misikitini, ambaye anaweza hata kukesha kanisani akakeshe hakuna atakayewafuata.”

Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa karibu na nyumbani kwake mjini Dodoma na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako alipatiwa matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa nchini Kenya.

Kwa takribani siku 10 sasa, Lissu amelazwa katika hospitalini nchini Kenya akiwa ICU baada ya kufanyiwa upasuaji mara tatu.

– PICHA: MTANDAO

MOTO: Nyumba ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, iliyopo Mwandiga, Kigoma ikiteketea kwa moto jana.

– PICHA: MTANDAO

UMOJA: Mbunge wa Singida Kaskazini,Lazaro Nyalandu CCM (wapili kushoto), akiwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (kushoto), Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema , Ezekiah Wenje, wakati alipofika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kumuona Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana hivi karibuni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.