WENGER KUENDELEZA UBABE KWA CONTE?

Mtanzania - - Mbele - LONDON, ENGLAND

UHONDO wa Ligi Kuu England utaendelea leo kwa michezo miwili mikali, Arsenal dhidi ya Chelsea ‘London derby’ na Manchester United watakaokuwa Old Trafford kucheza na Everton.

Mashabiki wa soka duniani kote wataweka historia ya kumshuhudia staa Wayne Rooney akirejea Old Trafford kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka na kujiunga na timu yake ya utotoni ya Everton.

Mbaya zaidi kwake ni kwamba, Man United wameshinda mechi 18 na kupoteza moja pekee kati ya 24 za Ligi Kuu walizokutana na Everton pale Old Trafford. Pia Everton imepoteza mechi nyingi za Ligi Kuu dhidi ya Man United kuliko timu nyingine yoyote.

Chelsea wataingia kwenye mchezo huo wakiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa wamejikusanyia pointi tisa, baada ya kushuka dimbani mara nne. Wakiwa wamecheza idadi hiyo pia, Gunners wako nafasi ya 11 kwa pointi zao sita.

Hata hivyo, kocha wa vijana hao wa Kaskazini mwa London, Arsene Wenger, amekuwa na rekodi nzuri katika mechi zake dhidi ya Antonio Conte.

Kwa mujibu wa takwimu, tangu Conte alipotua Stamford Bridge akitokea Italia alikokuwa akiinoa timu ya Taifa hilo, amejikuta akishindwa kutamba mbele ya Mfaransa huyo.

Licha ya msimu uliopita kunyakua ubingwa wake wa kwanza akiwa England, Conte ameshinda mara moja tu katika mechi zake nne alizokutana na Wenger, jambo linaloipa nguvu Arsenal katika mchezo wa leo.

Katika mchezo wa kwanza, Chelsea walichezea kichapo cha mabao 3-0 katika Uwanja wa Emirates. Ingawa Chelsea walilipiza kisasi katika mchezo wa marudiano, baadaye walipoteza mara mbili mbele ya wenzao hao.

Chelsea walichezea kichapo katika mchezo wao wa fainali ya Kombe la FA na kisha kushuhudia wakiukosa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa mikwaju ya penalti siku chache kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu England.

Rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimekutana mara 191 na ni Arsenal ndio wanaoongoza kwa kupata matokeo mazuri, wakiwa wameshinda mara 75, wakipoteza michezo 62 na kutoa sare 54.

Hata hivyo, rekodi hizo haziwapi Arsenal uhakika wa kushinda mchezo wa leo, ikizingatiwa kuwa, Chelsea wameonekana kukaa sawa baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Burnley katika mchezo wa ufunguzi.

Kichapo hicho kimewaacha usingizini vijana hao wa Conte, kwani wameshinda mechi zao zote tatu za Ligi Kuu zilizofuata, ukiwamo ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo mgumu dhidi ya Tottenham, katika Uwanja wa Wembley.

Katika mtanange wa leo, mashabiki wa Blues watafurahia uwepo wa staa wao mpya, Davide Zappacosta, ambaye aling’ara wakati walipoishindilia Qarabag mabao 6-0 mwanzoni mwa wiki hii.

Pia, tayari Gar Cahill amerejea baada ya kumaliza kuitumikia adhabu yake ya kukosa mechi tatu, huku Willian, Michy Batshuayi na Eden Hazard wakiwa fiti kuwavaa Arsenal.

Kwa upande wa mzee Wenger, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwafuata Chelsea, Alhamisi ya wiki hii aliwapumzisha mastaa wake saba katika mchezo wa Ligi ya Europa dhidi ya Cologne ya Bundesliga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.