Waajiri wanalalamikia wahitimu kukosa ujuzi - Majaliwa

Mtanzania - - Habari - Na RAMADHAN HASSAN –DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa waajiri kwamba wahitimu wengi wa ngazi mbalimbali za mafunzo wanaingia katika soko wakiwa hawana ujuzi unaohitajika.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa wakati alipokuwa akizindua miongozo ya mafunzo katika maeneo ya kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa, alisema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa waajiri kwamba wahitimu wengi hawana ujuzi.

Alisema jambo hilo husababisha waajiri kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Waziri Mkuu alisema jambo hilo wamelijadili kwa pamoja kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi na kukubaliana kuwa kuna tija ya kuhakikisha wanachochea na kuimarisha mfumo wa utoaji wa mafunzo.

Alisema kwa pamoja waliazimia kuandaliwa kwa miongozo ya kitaifa ya kusimamia mafunzo kwa vitendo na mafunzo ya uanagenzi.

“Lengo ni kuhakikisha mafunzo yatolewayo maeneo ya kazi yana ubora unaohitajika,” alisema.

Majaliwa alisema kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Alisema ripoti ya mwaka 2017 ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu hali ya ajira, inaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 201 sawa na asilimia 5.8 hawana kazi.

Pia alisema kwa upande wa Tanzania, utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 unaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini ni asilimia 10.3, kwa vijana ni asilimia 11.7.

Kwa upande wake, Mtendaji wa ILO Tanzania, Dk. Mary Kawar, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mambo mbalimbali.

– PICHA: OWM

UZINDUZI: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, Mary Kawar kitabu baada ya kuzindua Miongozo ya Mafunzo Katika Maeneo ya Kazi, Dodoma jana....

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.