‘Mapambano ya wanahabari, dola si ya muda mfupi’

Mtanzania - - Habari - Na AMINA OMARI –TANGA

MKURUGENZI wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura, amesema kuwa mapambano ya wanahabari dhidi ya dola si ya muda mfupi.

Kwamba ni mapambano ya kudunu hadi hapo watawala watakapotambua umuhimu wa vyombo vya habari na wanahabari.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa kukabidhi tuzo ya uandishi wa kishujaa na utumishi uliotukuka ya Daudi Mwangosi ambayo kwa mwaka huu ilikwenda kwa kituo cha Clouds TV.

Alisema kuwa mazingira ya wanahabari kikazi yamebadilika kutokana na mazingira ya kiutendaji, kisiasa kiutawala na mabadiliko ya kiteknolojia nchini.

“Mapambano haya si ya kumalizika mwaka mmoja, bali ni ya muda mrefu mpaka hapo watawala watakapoamua kwa dhati kutambua uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari nchini,” alisema Sungura.

Aliongeza kuwa mapambano hayo yataweza kwisha kama watawala watatambua umuhimu wa vyombo na waandishi wa habari katika kuchangia maendeleo ya nchi hii.

“Licha ya kazi kubwa tunayoendelea kuifanya, bado mchango wetu haujaweza kuonekana katika sekta mbalimbali licha ya kuibua mambo mengi ikiwamo rushwa na utawala bora.

“Kupitia vyombo vya habari ndipo kulipoweza kuibuliwa matukio mbalimbali ikiwamo tuhuma za rushwa katika bandari ya Dar es Salaam, lakini bado mchango wetu haujaweza kujulikana,” alisema Sungura.

Alisema kutokana na kutokuwapo kwa takwimu sahihi za mchango wa tasnia hiyo katika maendeleo ya nchi, TMF inatarajia kuanzia mwakani kufanya tafiti za mchango wa sekta hiyo kiasilimia.

Sungura alisema kuwa kupitia utafiti huo, wataweza kubaini ni taarifa gani imeweza kuchangia kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali nchini.

“Tunajua kila mara kumekuwa na takwimu zinazotolewa kuhusu michango ya sekta fulani kama afya elimu au mazingira, lakini huwezi kujua mchango wa waandishi katika kuleta maendeleo hayo,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.