Omog kumaliza unyonge kwa Mwadui

Mtanzania - - Habari - Na MOHAMED KASSARA

SIMBA inashuka dimbani leo kuikabili Mwadui FC katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara, litakalopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Kocha wa Simba, Joseph Omog, atakiingiza kikosi chake uwanjani huku akifahamu kwamba, anahitaji matokeo ya ushindi tu ili kuwashusha presha viongozi na mashabiki wa timu hiyo waliokwazwa na suluhu katika mchezo wao uliopita dhidi ya Azam.

Uongozi wa Simba pamoja na mashabiki wa klabu hiyo wamegawanyika kuhusiana na uwezo wa kocha huyo, upande mmoja ukiamini kwamba atawapa mafanikio, lakini mwingine unaona umefika wakati wa kufanyika mabadiliko katika benchi lao la ufundi.

Upande unaompinga kocha huyo unadai kutoridhishwi na mbinu zake za ufundishaji, kwani unaamini kikosi cha timu hiyo kina uwezo wa kumwadhibu mpinzani wao yeyote kutokana na kukusanya mastaa wenye uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu, kama washambuliaji Emmanuel Okwi na John Bocco pamoja na kiungo Haruna Niyonzima.

Kutokana na imani yao hiyo, uongozi umedaiwa kumpa kocha huyo mechi tano ambazo ndizo zitaamua hatima yake kama aendelee kupewa jukumu au atemwe na kutafutwa mwingine.

Uamuzi huo ulichukuliwa siku tano baada ya kikosi cha Wekundu hao kulazimishwa suluhu na Azam, katika mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu msimu huu, uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, wiki moja iliyopita.

Kwa mantiki hiyo, Omog anatakiwa kuhakikisha timu yake inashinda mechi nne zilizobaki, baada ya kukosa ushindi dhidi ya Azam.

Mechi hizo ni pamoja na hii ya leo dhidi ya Mwadui FC, nyingine ni dhidi ya Mbao FC itakayopigwa Mwanza, Singida United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma pamoja na Mtibwa Sugar itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mbali na presha hizo kwa Omog, Simba itaingia katika mchezo huo ikihitaji ushindi ili kuendelea kukimbizana na wapinzani wao, Yanga, kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Simba kwa sasa ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi nne, baada ya kucheza michezo miwili, ikianza kwa kuwacharaza Mafaande wa Ruvu Shooting mabao 7-0, kabla ya kulazimishwa suluhu na Azam FC.

Pia Simba itataka kuendeleza ubabe wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili kati ya timu hizo, uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Kama itafanikiwa kuvuna pointi tatu katika mchezo huo, itafikisha pointi saba na hivyo kuzidi kuchumpa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Kwa upande wake, Mwadui itaingia uwanjani ikiwa na shauku ya kuvuna ushindi ili kulipa kisasi hicho, lakini pia kufuta machungu ya kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, katika mchezo wao uliopita kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.

Mwadui ilizindua kampeni za Ligi Kuu msimu huu kwa kuichapa Singida United mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, kabla ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa, katika mchezo uliopita na kuifanya timu kukusanya pointi tatu hadi sasa.

Habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kurejea kwa Okwi, ambaye alikosekana katika mchezo uliopita kutokana na kuwa katika majukumu mengine katika timu ya Taifa Uganda ‘The Cranes’, iliyocheza mechi za kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Misri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.