‘Salaam ulimwengu wote kutoka Pyongyang’

Mtanzania - - Habari -

ANDIKO langu nimeliandika katika hali ya tofauti, hivyo msomaji wangu itazame fikra hii, naamini lipo jambo utajifunza. Endelea…

“Sisi hapa Pyongyang, Korea Kaskazini tunaendelea vema na “Military propaganda”. Kwanza tunawaambia waandishi wa habari wote hawaruhusiwi kupiga picha katika mazingira machafu. Tunawaambia wapige picha kwenye mazingira mazuri tu.

“Waandishi wa habari kokote wanakotembelea huambatana na askari kwa ajili ya ulinzi. Mojawapo ya ulinzi ni kuhakikisha hakuna eneo chafu linalotembelewa na mwandishi mgeni. Hivi ndivyo tunavyodhibiti habari zinazotuhusu.

“Aidha, hapa Pyongyang tunao makachero wetu ambao tumewafanya wawe wakurugenzi kwenye mashirika makubwa mbalimbali ili kuendesha uchumi na kudhibiti wapenyezwaji wowote wa kijasusi.

“Vilevile tumehakikisha tunafanya “recruitment” kwa vijana wote wenye sifa ya ujasusi na asili ya Pyongyang warejee nyumbani. Tunawaahidi maisha matamu na mazuri zaidi wakati wowote mtembeleapo nchi hii.

“Sisi tunajua tumetengwa, lakini hatulazimishi urafiki na nchi yoyote, ikiwamo Tanzania, iliyopo katika Bara la Afrika. Kama biashara tufanye biashara, kila mmoja ashike hamsini zake. Tunafanya mambo yetu kwa ufasaha na viwango. Wala hatumuudhi mtu, tuna amani mioyoni mwetu.

“Tatizo lenu mnadhani sisi ndio walengwa wa Marekani katika vita vya maneno vinavyoendelea. Tunakuambieni mkae mkitambua kuwa mlengwa wa kadhia hii ni China. Ndiyo maana mnaona wanasisitiza China waongee nasi hapa Pyongyang eti tusijaribishe wala kurusha makombora yetu.

“Kwani hamuoni wale maradikozi dhidi ya China wamepewa uwaziri au vyeo serikalini huko New York? Na yule aliyeandika vitabu namna ya “kuibutua China” kwa mashambulizi ya Sera na hila hamuoni yuko serikalini sasa? Ile serikali ya wafanyabiashara watupu na wengine ndo walioandika vitabu vya kiradikozi kabisa dhidi ya China.

“Kimsingi zifuatilieni China na Marekani. Hawa ndo wenye vita hivi. Sisi hatumo. Ila msiingie kwenye 18 zetu, maana maneno yetu dhidi yenu si vitendo vyetu.

“Nisikilizeni kidogo kwa mara nyingine, ninawapa salamu hizi kutoka mkoa mwingine. Sisi tumeingia mji wa Wonsan, uliopo kwenye jimbo la Kangwon hapa Korea kaskazini. Baada ya shughuli zetu kumalizika katika mji huo tunaelekea Chongjin uliopo kwenye Jimbo la Hamgyong.

“Stori iko hivi. Kwenye mji wa Wonsan kuna bandari ya kijeshi yetu sisi Korea Kaskazini. Hapa kuna silaha mbalimbali. Ukitaka mambo ya ‘Muzzle up’ au ‘Muzzle down’ uwe unahudhuria gwaride la kila mwaka la kijeshi liitwalo, “Kim II Jong; Day of the sun”. Kalaghabahoo! Ila kwenye bandari hii kuna silaha kali za nguvu. Kuna vifaru na kila silaha za kisasa kama mji wa Chongjin yaliko makombora mazito na makomandoo.

“Nyie mnahangaika kudhani tutawashambulia Marekani kwa makombora. Unajua sisi hapa Korea Kaskazini tunawalenga Korea Kusini? Hawa ndo tunawatafuta usiku na mchana. Siku tukichokozwa mengi yatafahamika. Sasa nyinyi mnadhani tunajihangaisha na mikwara bubu, na mbwembwe za hapa na pale eti tunaitafuta Marekani.

“Acheni hizo. Sisi tunaitafuta Korea Kusini, kama Russia wanavyoisaka Ukraine, Georgia au Poland. Kwani hamjui hapo Korea Kusini kuna ngome za kijeshi za Marekani?

“Kwani hamjui pale Poland kuna ngome ya kijeshi ya Marekani? Kwani hamjui pale Georgia na Ukraine pana ufadhili wa kijeshi wa Marekani? Sisi hapa Korea Kaskazini tunawaonyesha ‘utemi’ hao Korea Kusini, tunataka kuwatindua kabisa. Bila ngebe maisha hayaendi aiseee! Tutawabamiza wao sio Marekani.

“Stori iko hivi. Hao jamaa wamekaribisha ngome za adui yetu. Hivi adui yako akifanya mazoezi ya judo wewe utaenda kununua kashata na kahawa au utajifua pia?

“Sasa wao wanatumika kama nyenzo ya kututafuta sisi, China na Russia. Kwani hamjui kule Syria jamaa wamefurumsha zile dili za nyukilia za Russia? Russia hawa hawa walianza Iraq, wakafurumshwa. Wakaenda zao Iran, wakafurumshwa kidogo, japo China ana mkataba wa kijeshi miaka 30 pale Iran kwenye kamji fulani hivi.

“Sasa wewe’ unadhani huyu Mpayukaji wa New York atafurahia uwezo wetu usipomtegemea yeye na ubeberu wake wa kijeshi na kidiplomasia?

“Shtuka, vita ni biashara inayolipa sana! Sikwambii uingie vitani. Sisi Korea Kaskazini hatuogopi vita vya aina yoyote. Sasa basi, hawa Russia wakaenda Syria, ndio kimenuka.

“Juzi wakatangaza “No flyzone’ kuwakomesha Marekani. Bado hali ni tete kule, hakuna amani Syria na wala magaidi hawajatokomezwa.

“Nakukumbusheni hawa Russia ndo wanaisuka upya Belarus ujue. Kaa kitako, sikiliza, kuna siku nitakwambia. Belarus nayo inasukiwa nyukilia maana ninyi mnatufikiria sisi Korea Kaskazini tu.

“Sisi kwanza hatuombi hela zenu kama nyie mlivyozoea kuomba omba kwa Marekani huko. Tunalima wenyewe, msitubabaishe! Kwani mtu asiyeomba misaada ya chakula, soda, biskuti au juisi Marekani ni adui yake?

“Mnataka tuombe ombe mpaka lini? Acheni unaa kabisa. Nchi inajengwa kwa sera zake, si zile za kuazima na kuomba kutoka kwa mabeberu ambao kwa namna moja au nyingine wanachotaka ni hali ya sisi kuendelea kuwategemea wao. Nimesikia mnaichunguza Tanzania kuagiza silaha kutoka kwetu.

“Sisi tunasema endeleeni kuchunguza, kwani ni haki na laiki yenu kufanya hivyo. Hatuna wasiwasi, tutazungumza nao kidiplomasia na tutalimaliza kidiplomasia.

“Nawaageni kwa leo. Huku jina langu la bandia ni Markus Lee Kim-jae. Nipo Mkoa wa Chongjin, Korea Kaskazini.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.