Wanenguaji wameishiwa ubunifu?

Mtanzania - - Habari -

NI jambo la kushangaza sana kwenda kwenye kumbi za starehe, hususan muziki wa dansi na kukosa burudani uliyoitaraji. Si kwa muziki mbovu au mazingira yasiyoridhisha, la hasha, kinachozungumzwa hapa ni upande wa waburudishaji, yaani wanenguaji.

Kimsingi, wanenguaji wa muziki wa dansi wa kipindi hiki wameonekana kukosa ubunifu kabisa. Achilia mbali kuiga unenguaji wa wenzao wa nchi ya Kongo na baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi, siku hizi hakuna jipya kwenye idara ya minenguo karibu katika bendi zote nchini.

Ni vigumu kulinganisha ubora wa wanenguaji wa bendi zetu na wenzao wa nje, kwani kadri siku zinavyosonga ndivyo wanavyozidi kushuka viwango na kushindwa kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa bendi zao.

Kifupi, siku hizi wanenguaji wanafanya kazi zao kwa mazoea, hakuna ufanisi kabisa. Ushahidi uko wazi, kama utapata muda wa kuhudhuria maonesho ya bendi zetu.

Hii si hukumu au tuhuma kwa wanenguaji, bali hali halisi ilivyo kwa kulinganisha jitihada za madansa (wanenguaji) wa miaka mingi iliyopita ambao kila kukicha walionesha ubunifu kwa kuweka vionjo mbalimbali na kuifanya fani hiyo kuwavutia zaidi wapenzi wa bendi zao. Mifano ya bendi za African Stars, FM Academia ya kipindi hicho inathibitisha.

Ndiyo maana tunajiuliza, wanenguaji wameishiwa ubunifu? Au wamekuwa wavivu, wazembe au wanakosa motisha toka kwa wamiliki wa bendi zao? Majibu yote wanayo wahusika ambao ni wanenguaji wenyewe na wanaomiliki au kuendesha bendi hizo.

Sina uhakika kama wameshalitupia jicho tatizo hili zaidi ya kuendelea kujiuliza eti kwa nini muziki wa dansi unaanguka? Ajabu sana!

Japo kuna mengi yanayochangia ku¿¿a kwa nguvu ya muziki wa dansi nchini kwa miaka ya karibuni, safu hii inapenda kuwashauri wamiliki na waendeshaji wa bendi kukutana na kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha wanaurejeshea hadhi na nguvu yake kama ilivyokuwa huko nyuma.

Hili linawezekana kabisa kama wataweka nia ya dhati.

Kwa leo naishia hapa, nawasihi wanenguaji kujaribu kuwa wabunifu na kujiongeza kwa kudokoa hapa na pale kwenye mitindo ya uchezaji kutoka makabila zaidi ya 100 ya Tanzania ambayo yamesheheni ‘staili’ tofauti za uchezaji zinazovutia mashabiki, kama wafanyavyo Wakongo ambao hutoa makabila ya kwao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.