Jukata waibukia tukio la Lissu kupigwa risasi

Mtanzania - - Habari / Tangazo - FARAJA MASINDE Na MANENO SELANYIKA -DAR ES SALAAM

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA), limelaani tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, lililotokea Septemba 7, mwaka huu na kuvitaka vyombo vya dola kufanya kazi yake ili wahusika wafikishwe mahakamani.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema ni fedheha kwa taifa linalojulikana kuwa kisiwa cha amani na utulivu, kutokea shambulio dhidi ya kiongozi bila kuwa na hatia.

“Ni kitendo cha ukatili wa kinyama alichofanyiwa Lissu mchana kweupe, kila mtu anafahamu kuwa mheshimiwa ni mtetezi wa wanyonge, hivyo tunaomba vyombo vya dola vifanye kazi yake na kubaini wahusika wa matukio ya aina hiyo,” alisema Mwakagenda.

Alisema hata kama angekuwa mwananchi wa kawaida angepigwa idadi ya risasi hizo, wao kama Jukata wangezungumza kwani ni utamaduni wao, hivyo wanamwombea mbunge huyo kwa Mwenyezi Mungu apone, kisha arudi na kuendelea katika majukumu yake ya kuwatumika wananchi wanyonge.

Kuhusu Katiba mpya, Mwakagenda alisema wamefuatilia kisha kuchambua Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria tangu mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2018 na kubaini kuwa Serikali bado haijatenga fedha zozote kwa ukamilishwaji wa mchakato wa upatikanaji wa katiba hiyo.

Alisema matumaini ya Watanzania yalikuwa kwamba katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, mchakato wa Katiba mpya ungeweza kukamilishwa, lakini hadi sasa matumaini yamekuwa ni hafifu.

“Hii ni bajeti ya pili sasa, ila hakuna fungu lolote angalau ile ya mwaka jana waliandika kwa maneno ila msimu huu hata yale maneno yameondolewa, ushauri wetu kwa mwaka huu tutapeleka bajeti ya dharura, ikishindikana masuala ya Katiba tusahau kwa sababu mwakani kutakuwa na maandalizi ya chaguzi mbalimbali ukiwemo Uchaguzi Mkuu wa 2020,” alisema Mwakagenda.

Alitaja kasoro sita ambazo zinatakiwa kushughulikiwa katika mapendekezo ya maboresho yanayohusu Tume ya Uchaguzi angalau uchaguzi wa Tanzania ungefanana na Kenya.

Alitaja maboresho hayo aliyosema kuwa yatasaidia kupanua demokrasia nchini kuwa ni pamoja na uhuru kamili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ile ya Zanzibar na fursa ya mgombea huru.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.