TRL kusitisha safari mbili wiki ijayo

Mtanzania - - Habari / Tangazo - Na Grace Shitundu

KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) imefuta safari mbili za treni yake inayokwenda Mwanza na Kigoma wiki ijayo, kupisha marekebisho ya uboreshaji wa miundombinu ya reli baada ya kuharibiwa na mvua zilizonyesha Mei 13, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa TRL, Focus Sahani, alisema mvua hizo zilisomba daraja lililopo kati ya stesheni ya Morogoro na Mazimbu.

Alisema awali daraja hilo lilifanyiwa matengenezo ya dharura na kwa sasa kwa tathmini ya kiufundi iliyofanyika, imeonekana ni hatari kuendelea kupitisha treni katika eneo hilo bila kuliimarisha zaidi.

“Uongozi wa kampuni umeona ni muda mwafaka sasa kulifanyia marekebisho madhubuti, hivyo imefanya marekebisho ya ratiba kufanikisha hilo.

“Hivyo ile treni yetu ya abiria ya siku ya Jumanne Septemba 19, inayotoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na Kigoma na ile ya Alhamisi Septemba 21 inayotoka Kigoma na Mwanza kwenda Dar es Salaam, hazitakuwepo kama kawaida,” alisema.

Alisema hata hivyo ratiba nyingine zinabaki kama kawaida na kuwaomba abiria na wananchi kuzingatia hilo ili waendelee kutoa huduma za uhakika na usalama unaostahili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.