Sikubaliani na wanaomtumia Rais Magufuli

Mtanzania - - Tahariri - Na ABRAHAM GWANDU - ARUSHA

Yapo baadhi ya mashirika na taasisi wanajaribu kujitangaza kupitia sauti na picha ya rais

TAASISI kadhaa za umma na binafsi, kwa muda sasa zimekuwa zikiendelea kutoa matangazo ya kudai kodi, kukumbusha wajibu, kukataza na kuonya juu ya masuala kadhaa kwa kutegemea sauti na maagizo mbalimbali aliyowahi kutoa Rais Dk. John Magufuli katika hotuba zake.

Ifahamike kuwa kutengeneza tangazo la biashara ni ubunifu maalumu ambao ni kazi ya watu wenye utaalamu huo, wenye lengo la kutangaza bidhaa na huduma inayopatikana kutoka kwa anayetangazwa.

Kutengeneza matangazo ni gharama, pia wabunifu huumiza vichwa kuyaandaa, ndiyo maana wanalipwa fedha nyingi kutokana na ubunifu wao.

Binafsi natia shaka iwapo wataalamu wanaomtumia rais wetu katika matangazo yao kama wamefanya kazi yao vizuri na kustahili kulipwa fedha, hasa katika mashirika ya umma.

Nimejaribu kudodosa kujua iwapo kufanya hivyo ni kosa kisheria, jawabu ni kwamba si kosa iwapo tu anayetumia sauti au picha husika alimshirikisha mwenye hiyo sauti na picha katika kutengeneza tangazo la kuhamasisha jambo fulani likiwamo la biashara.

Yapo baadhi ya mashirika na taasisi wanajaribu kujitangaza kupitia sauti na picha ya rais pale anapozitaja taasisi zao katika hotuba zake au anapokuwa akitoa maelekezo mahususi yanayohusu taasisi na mashirika husika.

Naamini zipo njia nyingi ambazo zinaweza kutumiwa na watangazaji kufikisha ujumbe bila kumtumia rais.

Kitendo hiki kinaibua maswali juu ya uwezo na ubunifu wa wanaoandaa matangazo.

Hadhi ya rais ni kubwa mno. Jambo hili likiachwa kuendelea likaota mizizi, haitashangaza kuona picha na sauti ya rais ikitumika katika mambo yasiyofaa. Ni mtazamo wangu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.