Kwaheri Muhingo historia itaishi

Mtanzania - - Jicho Pevu - Na VENANCE RWEGOSHORA

SEPTEMBA 3, mwaka huu, nikitoka Bukoba kuelekea Mwanza, nikiwa kwenye mji mdogo maarufu, Chato, nilinunua nakala ya gazeti moja linalochapishwa kila siku na kusoma taarifa iliyonishtua kuhusu kifo cha rafiki yangu Muhingo Rweyemamu.

Katika andiko hilo mwandishi wa habari alieleza wasifu wa marehemu, tunaomfahamu Muhingo wasifu ulikuwa na mapungufu.

Marehemu Muhingo hakuwa na miaka 67 kama ilivyoandikwa, bali siku aliyozikwa ndiyo alikuwa anatimiza miaka 59 kamili.

Upungufu mwingine mwandishi alisahau kutaja kuwa Muhingo alipata kuwa Mhariri wa Gazeti la Tanzania leo mwaka 1999 hadi mwanzoni mwa mwaka 2000.

Yawezekana mwandishi hakutaja kwa kuwa gazeti hilo halipo mitaani kwa muda mrefu sasa.

Licha ya kutokuwapo kwa gazeti hilo, hata hivyo hakuondoi ukweli kwamba nakala zake nyingi bado zipo kwenye makabrasha mbalimbali yaliyohifadhiwa majumbani, maofisini au maktaba.

Tanzania Leo ni gazeti lililopata usajili na kuchapisha matoleo takribani 500, hivyo si rahisi kufutika. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kazi ya fasihi si ya kufa.

Ni wazi kuwa mtu aliyefanya kazi yoyote ya kifasihi hawezi kusahaulika kamwe.

Napenda nikiri hapa kwamba mimi sikupitia katika shule rasmi za undishi wa habari. Hata hivyo nimebahatika kukaa katika vyumba vya habari kwa mrefu kutokana na kazi yangu.

Nilipata kufanya kazi na waandishi mahiri, akiwamo Muhingo Rweyemamu (marehemu), Salva Rweyemamu, Jenerali Ulimwengu, Dk Gideon Shoo, Stanley Kamana (marehemu), Jesse Kwayu, Francis Chirwa na wengine wengi.

Baadhi ya vyombo vya habari ambavyo nimepata kuvifanyia kazi ni pamoja na The Express, Mwananchi ya mwanzo, The Guardian Nipashe, Habari Corporation na Tanzania leo.

Ingawa kazi yangu haikuwa ya uandishi kama nilivyoeleza awali, hata hivyo nilijifunze baadhi ya vitu vya msingi katika tasnia ya habari ili niweze kwendana na mazingira husika.

Kama tunavyofahamu kazi kuu ya kwanza ya vyombo vya habari ni kuhabarisha, kuelimisha na kukosoa. Mimi nilikuwa nashughulika na sehemu ya pili ya magazeti upande wa biashara.

Muktadha wa makala haya ni kumwelezea ninavyomfahamu Muhingo kupitia taaluma ya habari, hasa alipokuwa ndani ya chumba cha habari, kazi zake za uandishi na uhariri alizozitoa katika gazeti la Tanzania leo na katika magazeti mengine.

Mimi ni kama Muhingo, sote tumepitia fani ya ualimu, tumepata kukutana katika vyuo kadhaa, baada ya masomo tulipoteana kwa muda, tulikutana kwenye vyumba vya habari, yeye akiwa mwandishi, mimi nikiwa upande wa biashara, yaani matangazo na usambazaji.

Muhingo alikuwa mwandishi mwenye upeo mkubwa wa kufikiri na kuandika habari iliyokuwa na sifa zote za kiuandishi, zilizofanywa katika misingi ya kiuchunguzi, ukweli na hakuwa na hulka ya woga, alikuwa jasiri na mbunifu. Katika habari zake alikuwa anatoa fursa kwa pande zote husika ‘balanced’ kabla haijachapishwa gazetini.

Habari aliyoiandika Muhingo ilikuwa inamvutia msomaji kutokana na staili ya uandishi wake. Kwa hiyo chumba cha habari cha Muhingo kilijaa kila aina ya changamoto kwa waandishi wenzake akitaka watafute habari zenye sifa hizo.

Katika hoja yangu ya ubunifu nitolee mfano wakati tukiwa kwenye Kampuni ya Habari Corporation, Muhingo alibuni na kuanzisha kijarida ndani ya gazeti la MTANZANIA Jumapili, kilichoitwa Jarida Maridhawa. Kijarida hicho kilisheheni habari za kijamii zaidi zilizovutia wasomaji wengi.

Muhingo aliwahi kufanya mahojiano na mwanamke mmoja aliyehukumiwa kifungo cha miaka 10 na kutumikia kifongo cha miaka sita baada ya kubainika hakukuwa na ukweli kuhusu kesi iliyokuwa inamkabili.

Kisa hicho kilikuwa kimeandikwa ka- tika staili ya kuvutia, licha ya kwamba kilikuwa kinasikitisha.

Kutokana na nafasi yangu ya masoko, nami nilibuni mbinu ya kutangaza redioni habari za gazeti letu zilizokuwa zinavutia magazetini.

Kutokana na habari ya mwanamama huyo, nililazimika kuongeza nakala 5,000 zaidi katika usambazaji wetu wa kila siku.

Pamoja na ongezeko hilo, kufikia saa tano asubuhi hapakuwapo na nakala ya gazeti letu mitaani. Hiyo ndiyo aina ya uandishi aliokuwa nao Muhingo, ambao kimsingi uliturahisishia kupata soko.

Nilipoachana na Kampuni ya Habari na kuanzisha gazeti la Tanzania leo, Muhingo aliungana nami bila kujali kuwa anaacha kazi kwenye kampuni kubwa, tulishirikiana hadi gazeti hilo likasimama.

Miongoni mwa habari kubwa ambayo leo hii inanifanya nizidi kumkumbuka Muhingo ni ile ya kuugua, kufariki na kuzikwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hata kauli yake ya mwisho kabla ya kufariki.

Tanzania leo ndilo lilikuwa gazeti pekee lililoandika tatizo na ugonjwa uliokuwa unamsumbua Mwalimu, pia lilifahamu hali yake wakati anapelekwa mjini London, Uingereza kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya St. Thomas.

Ni gazeti hilo hilo ndilo liliandika hospitali (St. Thomas), alipokuwa amelazwa Mwalimu Nyerere na kuibua mjadala kuwa taarifa hiyo haikuwa na ukweli na kulitia matatani gazeti hilo.

Hata tulipoitwa Idara ya Habari (Maelezo), Muhingo alisimamia msimamo wake kuwa habari hiyo haikuwa na chembe ya uongo, kwani ilitolewa na chanzo cha kuaminika ‘Impeccable source’, nami nikacheza humo humo ingawa ilikuwa mara ya kwanza kusikia neno hilo!

Ubunifu na utundu wa Muhingo katika tasnia ya habari ulikuwa mkubwa, katika gazeti hilo alipata kuchapisha picha ya Chifu Nyerere Burito, baba mzazi wa Mwalimu Julius Nyerere.

Ama kwa hakika mambo ya Muhigo Rweyemamu yanaweza kujaza kurasa nyingi za vitabu na magazeti. Nimeona niandike haya ili waandishi wanaochipukia wajue umuhimu wa kuwajibika ipasavyo katika vyumba vya habari.

Aidha, nimeona ni vyema nikaonyesha upande mwingine wa gazeti unahitaji nini.

Mimi niliyekuwa upande wa biashara wa gazeti nathubutu kusema nilipata furaha na bahati ya kufanya kazi na mwandishi nguli Muhingo Rweyemamu. Niseme ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari, umri wake ulikuwa unaruhusu kufanya makubwa zaidi. Kikubwa ni kumuenzi kwa kuyakuza aliyoyaanzisha na kuyapigania.

Pale makaburini Kinondoni wakati tukimpumzisha, rafiki yake mkubwa, Absalom Kibanda, aliteta na mimi na kuniambia kwamba marehemu alikuwa ameniongelea na gazeti la Tanzania leo.

Ingawa sikuuliza undani wa habari hiyo, lakini naweza kubashiri kwa uhakika kwamba, Muhingo alikuwa na mawazo ya kuona jinsi tunavyoweza kulirudisha mtaani gazeti la Tanzania leo.

Naamini kuna siku gazeti letu litarudi mtaani na kuwapata wanaojituma kama alivyokuwa Muhigo.

Umeondoka Muhingo, nakulilia, sitaacha kukukumbuka.

Habari aliyoiandika Muhingo ilikuwa inamvutia msomaji kutokana na staili ya uandishi wake. Kwa hiyo chumba cha habari cha Muhingo kilijaa kila aina ya changamoto kwa waandishi wenzake akitaka watafute habari zenye sifa hizo.

Buriani Muhingo Rweyemamu.

Rweyemamu Muhingo enzi za uhai wake

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.