Mtuhumiwa wa ujambazi auawa na wenzake Dar

Mtanzania - - Habari - Na UPENDO MOSHA

MTU mmoja anayedaiwa kuwa ni jambazi aliyefahamika kwa jina la Robert Massawe (51), mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni washirika wake.

Masawe aliuawa na wenzake hao Oktoba 8, mwaka huu, kati ya saa 10 na saa 11 alfajiri, katika Kijiji cha Chilio, Wilaya ya Rombo, katika tukio la ujambazi wakati wa majibizano ya risasi baina yao na askari polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba, marehemu alikamatwa Oktoba 4, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, akihusishwa na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha na kusafirishwa hadi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya upelelezi. “Baada ya mtu huyo kufikishwa hapa Kilimanjaro, alitoa ushirikiano kwa polisi kwa kutaja matukio ya ujambazi ambayo wamewahi kuyafanya katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu pamoja na kuonyesha walikoificha bunduki aina ya SMG yenye namba za usajili 1996 AFU 2761, iliyokuwa imefukiwa ardhini katika eneo la Kata ya Kaloleni, jirani na Kiwanda cha Ngozi.

“Baada ya kuonyesha silaha hiyo Oktoba 5 mwaka huu, aliendelea kutoa ushirikiano kwa polisi na kutoa taarifa ya kuwapo kwa mpango wa tukio la ujambazi lililotarajiwa kufanyika Oktoba 8, saa tisa usiku, katika Kijiji cha Chilio, Kata ya Holili, katika Kiwanda cha Saruji Moshi.

“Katika maelezo yake, alieleza mpango wa tukio la ujambazi ambalo walikuwa wamepanga kulifanya na alipokwenda na polisi eneo husika, alipiga kelele na kusema kuna polisi mahali hapa.

“Baada ya kupiga kelele, majambazi wenzake walianza kukimbia huku wakipiga risasi hovyo katika harakati za kujihami wasikamatwe, ndipo baadhi ya risasi zilimpata mwenzao katika mkono wa kushoto, mgongoni na kwenye mguu wa kulia.

“Majeraha hayo yalisababisha kifo chake wakati akipelekwa hospitalini kwa sababu alivuja damu nyingi sana.

“Awali, tulipekua nyumbani kwake Dar es Salaam na kukuta simu 19 za aina tofauti, betri tisa za simu pamoja na laini za simu zaidi ya 50. “Pamoja na mtuhumiwa huyo kuuawa, mke wake tunamshikilia huko Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kufanikisha jitihada za kuwakamata wote walioko kwenye mtandao huo wa kijambazi,” alisema Kamanda Issah.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.