Messi aipeleka Argentina Kombe la Dunia

Mtanzania - - Habari - QUITO, ECUADORW

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, amefanikiwa kuipeleka timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, baada ya kuifungia mabao matatu dhidi ya Ecuador.

Argentina ilishinda mabao 3-1 huku mshambuliaji huyo akipiga ‘hat trick’ huku timu hiyo ikitokea nyuma na kuibuka na ushindi.

Katika mchezo huo wa juzi, Argentina walianza huku wakiwa wanashika nafasi ya sita katika msimamo, hivyo walikuwa hatarini kutofuzu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1970.

Wenyeji wa mchezo huo, Ecuador walijiweka kifua mbele baada ya sekunde ya 38 kufunga bao kupitia kwa mshambuliaji wao, Romario Ibarra, bao hilo lilikuwa la mapema sana kufungwa kwenye michuano hiyo.

Argentina ambao walimaliza wa pili Kombe la Dunia nchini Brazil 2014, walijikwamua baada ya Messi kuanzisha mashambulizi na mshambuliaji mwenzake, Di Maria na kisha kugongeana huko kukampa nafasi mchezaji huyo ya kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 12.

Hata hivyo, dakika nane baadaye mchezaji huyo aliongeza bao la pili kwa shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni, dakika 45 zilimalizika huku Argentina wakiwa mbele kwa mabao 2-1, lakini baada ya kipindi cha pili kuanza nyota huyo aliendelea kuliwinda lango la wapinzani wao na kufanikiwa kupachika bao lake la tatu.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Messi alisema ingekuwa jambo la kushangaza sana endapo Taifa lake lingeshindwa kufuzu michuano hiyo mwakani.

“Tulikuwa kwenye wakati mgumu sana wa kuweza kufuzu, jambo ambalo lilikuwa linaniumiza sana kichwa kila wakati, lakini tunamshukuru Mungu tumefanikisha malengo yetu kutokana na jinsi tulivyopambana.

“Lingekuwa jambo la kushangaza sana endapo tungeshindwa kufuzu michuano hiyo, mara ya mwisho tulifika hadi fainali na kumaliza nafasi ya pili, kwenye michuano ya Copa America tumefika fainali mara mbili mfululizo, hivyo ingeshangaza sana kushindwa kufuzu,” alisema Messi.

Timu ambazo zimefanikiwa kufuzu upande wa Amerika ya Kusini ni pamoja na Brazil ambayo ilikuwa ya kwanza, Uruguay ya pili, Argentina inashika nafasi ya tatu huku nafasi ya nne ikishikwa na Colombia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.