Mahakama yataka ushahidi Mdee kumkashifu JPM

Mtanzania - - Habari/Tangazo - Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeutaka upande wa Jamhuri kuita mashahidi Novemba 8, mwaka huu kueleza jinsi Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alivyomkashifu Rais Dk. John Magufuli.

Mahakama ilifikia uamuzi huo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, baada ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kukana kumkashfu Rais Magufuli.

Mdee alikana kumwambia Rais Magufuli kwamba “anaongea ovyo ovyo , anatakiwa afungwe breki” kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa Amani.

Pia alikana maelezo ya Jamhuri kwamba akiwa katika mahojiano Kituo cha Polisi Kibangu alikubali kutenda makosa hayo.

Baada ya kukana, Hakimu Nongwa alisema kwa yale aliyokataa kutenda, upande wa mashtaka unatakiwa kupeleka mashahidi.

Jamhuri ikiongozwa na Wakili wa Serikali, Leonard Challo ilikubali kupeleka mashahidi Novemba 8, 2017 kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wao.

Katika kesi hiyo, Halima anadaiwa kuwa alifanya kosa hilo Julai 4,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni.

Anadaiwa kumtukana Rais John Magufuli kwa kusema “anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki” kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mdee anawakilishwa mahakamani na Wakili Hekima Mwasipu.

– PICHA: IMANI NATHANIEL

MAHAKAMANI: Watuhumiwa wa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi katika Chuo cha Uhasibu wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kusomewa mashitaka yanayowakabili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.