Waziri Kairuki: Sitasahau uhakiki watumishi hewa

Mtanzania - - Habari/Tangazo - Na AGATHA CHARLES

WAZIRI wa Madini, Angellah Kairuki, amesema suala la uhakiki wa watumishi hewa ni moja ya changamoto kubwa aliyopambana nayo alipokuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kairuki alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipokuwa akikabidhi taarifa za kazi kwa Waziri mpya wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu, George Mkuchika.

Alisema ingawa suala la uhakiki lilikuwa ni gumu, lakini lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa licha ya baadhi ya maofisa utumishi kutokuwa waaminifu na kushirikiana na watumishi kudanganya.

“Uhakiki ulikuwa mgumu, nchi kama India na Afrika Kusini walifanya kwa awamu nne na hawakumaliza. Sisi tumefanya vema, naipongeza Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa).

“Maofisa utumishi wengine hawakuwa waaminifu, walishirikiana na watumishi kudanganya, kama kuna masalia mengine naamini yataondolewa,” alisema Kairuki.

Alisema changamoto nyingine aliyokumbana nayo na kuomba Mkuchika kuendelea kuifanyia kazi ni maslahi ya watumishi kulingana na gharama za maisha.

Alisema alianza na awamu ya kwanza kurejesha nidhamu na kuondoa watumishi hewa na kulinda maadili ya utumishi wa umma.

Alisema changamoto nyingine ambayo hata hivyo alifanikiwa kukabiliana nayo ni ukubwa wa wizara hiyo ambayo iliunganishwa kutoka nyingine tatu na kuwa moja.

Akizungumza kabla ya kukabidhiwa taarifa za kazi, Mkuchika ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, pamoja na kumshukuru Kairuki, alisema atazungumza na Waziri wa Elimu ili kuweka mtaala wa somo la rushwa kuanzia ngazi ya shule za msingi.

“Nitaongea na Waziri wa Elimu kuwapo mtaala wa elimu ya rushwa kuanzia shule za msingi. Kazi kubwa ni uelewa wa wananchi juu ya rushwa, wataalamu wa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) waalikwe kutoa elimu,” alisema Mkuchika.

Mkuchika alisema nchi za Scandinavia zikiwamo Norway na Sweden zilifanikiwa kupunguza rushwa kwa kutoa elimu.

Kuhusu nidhamu, Mkuchika alisema kuna wakati iliporomoka tofauti na miaka iliyopita ambako watumishi wa umma walitambuliwa kwa sifa hiyo.

Akitoa pongezi zake kwa Kairuki kuchaguliwa kuongoza Wizara ya Madini, Mkuchika alisema pamoja na kusoma orodha kwenye gazeti, ya mawaziri waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini na hawakuwa salama, ana imani waziri huyo atafanikiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.