Tatizo la mimba kwa wanafunzi lidhibitiwe

Mtanzania - - Tahariri -

TATIZO la wanafunzi kupata ujauzito katika maeneo mbalimbali nchini, limekuwa ni ajenda ya kitaifa kila kukicha. Jambo hilo husababisha wanafunzi wengi wa kike, kukatishwa ndoto zao za masomo kutokana na watu wasiokuwa na nia njema kwao.

Tatizo hili limezidi kukuwa siku hadi siku, kutokana na kuwapo takwimu nyingi zinaozoonesha kila mwaka idadi ya wanafunzi wa kike wanavyoshindwa kuhitimu elimu ya msingi au sekondari.

Kutokana na hali hiyo, Serikali na wadau wengine wamekuwa mstari wa mbele kupaza sauti ya namna ya kupambana na tatizo hili, lakini hali bado imezidi kuwa mbaya.

Leo tumelazimika kusema haya baada ya kushtushwa na taarifa kuwa Mkoa wa Katavi ndio unaoongoza kwa tatizo hilo kwa asimilia 45 kitaifa. Hii ni hali ya hatari kama hatua hazitachukuliwa.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga, amesema kuanzia sasa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali watu watakaowapa mimba wanafunzi.

Habari hii ni mbaya kwa watu ambao hawawatakii mema wanafunzi hawa ambao ni viongozi wa taifa la kesho. Hatuwezi kuwa na taifa ambalo wataalamu watarajiwa wanakatishwa ndoto zao.

Tunaamini kauli hii ya RC Muhuga imekuja baada ya kuona namna tatizo hili kwa wanafunzi likizidi kupanda siku hadi siku.

Anasema takwimu zinazoonesha mkoa wake unaongoza kitaifa kwa mimba za utotoni kutokana na matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria kwa mwaka 2015-2016.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 45 ya wasichana wa umri wa miaka 15 hadi 19 , wameanza kuzaa, huku asilimia 33.3 wakiwa wamezaa angalau mtoto hai mmoja.

Aidha takwimu zinaonyesha asilimia 11.8 walikuwa wajawazito. Mkoa wa Katavi ukiwa ni moja ya mikoa nchini yenye kiwango kikubwa cha mimba za utotoni katika kipindi cha miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2012-2016 na kusababisha wanafunzi 258 wa shule za msingi na sekondari kukatiza masomo yao kutokana na ujauzito.

Kwa mujibu wa takwimu hizo wanafunzi 494 kati ya 14,127 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi hawakufanya mtihani. Kati ya hao wasichana 220 wakiwa wajawazito.

Lakini hali hiyo, pia ipo kwa elimu ya sekondari ambapo, wanafunzi 123 walishindwa kufanya mtihani wa kuhitimu, kati ya 6,284 waliosajiliwa kwa kipindi cha mwaka 2014/16 kwa sababu mbalimbali, ikiwemo mimba. Pia matatizo ya aina hii yameshamiri katika mikoa karibu yote na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kupambana na tatizo bila kuchoka hata kidogo na mamlaka zinazohusika zionyeshe makali yake.

Sisi MTANZANIA, tunamshauri RC Muhuga kuwa kiwango hiki ni kikubwa na kinahitaji kuchukua hatua za haraka kwa kushirikiana na mamlaka zingine ndani ya mkoa huu. Haiwezekani Taifa liendelee kupoteza wataalamu wa kesho ambao wanaweza kuja kuwa wakombozi wa baadae.

Lakini pia tunashauri RC Muhuga kuona umuhimu wa kuhamasisha wananchi wa mkoa wake kuanza haraka ujenzi wa mabweni ya shule hasa kwa upande wa wanafunzi wa sekondari, kufanya hivi kutasaidia mno kupunguza tatizo hili.

Tunatambua namna ambavyo mazingira magumu na vishawishi vingi wanavyowazunguka watoto wa kike, lakini lazima Serikali na jamii wapambane navyo bila kuchoka. Ndiyo maana tunasema RC Muhuga chukua hatua takwimu hizi zinatisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.