Tusikubali vitendo hivi viote mizizi nchini mwetu

Mtanzania - - Tahariri - Na VERONICA ROMWALD

HAKUNA ubishi kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani. Tangu enzi za mababu zetu watu wamekuwa wakiishi kwa kuaminiana na kupendana.

Utulivu uliopo unaing’arisha Tanzania hadi nje ya mipaka yake, wengi wakivutiwa kuja kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo tumejaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa mfano, tumejaliwa mlima mrefu kuliko yote barani Afrika (Kilimanjaro), mbuga za wanyama, mito, maziwa, maliasili za kila aina, madini ambayo hayapatikani kwingineko duniani na wanyama wa kila aina wanaopatikana ndani ya nchi yetu.

Hakika inavutia, ikiwa umebahatika kufanya utalii katika vivutio mbalimbali tulivyojaliwa kuwa navyo nchini, basi utaungana na mimi katika kueleza uzuri wa Tanzania.

Ni wazi kwamba, utalii unasaidia kukuza uchumi wa Taifa letu na hivyo ni muhimu kuilinda amani iliyopo na kuidumisha na si vinginevyo.

Kwa siku kadhaa, yamekuwa yakiripotiwa matukio ambayo hayapaswi kufumbiwa macho, kwa mfano vitendo vya mauaji, utekaji nyara yametikisa Taifa letu na kuacha majonzi.

Kwa namna moja au nyingine, napenda kuvipongeza vyombo vya dola kupitia viongozi wenye dhamana na masuala ya ulinzi ambao wamesisitiza kwamba, watahakikisha wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kujibu mashtaka yao.

Ni jambo linalofariji na kuona jinsi ambavyo viongozi wanahakikisha suala hilo linafanyiwa kazi, kwani kuliacha na kukaa kimya ipo siku matukio haya yataota mizizi. Binafsi sipendi tufike huko na ndiyo maana navipongeza kwa hatua walizoanza kuchukua, lakini pamoja na hayo, kuna jambo jingine ambalo linasumbua akili zetu.

Katika siku za hivi karibuni, iliripotiwa kwamba Jeshi la Polisi limeokota miili huko katika ufukwe wa bahari.

Miili hiyo ilikutwa ikiwa kwenye viroba na bado hatujaelezwa ni ya kina nani. Aidha, usiku wa juzi katika mtandao mmoja wa kituo kimoja cha redio iliripotiwa kuokotwa kwa mwili mwingine huko katika ufukwe wa bahari, eneo la Kawe.

Kujirudia kwa matukio haya kunazidi kutupa hofu na wasiwasi mkubwa wananchi, kwamba nani ambaye anahusika na vitendo hivi.

Tunajiuliza kwanini miili inaokotwa huko ufukweni, wauaji wanafanya hivyo kwa nia gani, nani amewatuma, wanapata faida gani kupoteza maisha ya wengine?

Ni maswali ambayo hatuna majibu sahihi hivi sasa, lakini ni vizuri Jeshi letu likafanya uchunguzi kwa makini na kwa haraka ili tujue adui yetu ni nani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.