Kesi ya kachero anayemshtaki IGP kusikilizwa Feb 2018

Mtanzania - - Kanda - Na JUDITH NYANGE

KESI ya aliyekuwa kachero Jeshi la Polisi katika Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Manga Msalaba, ya kudai malimbikizo ya mshahara wa miezi 33 imepangwa kuanza kusikilizwa Februari 8, mwaka 2018.

Msalaba anadai hakulipwa mishahara hiyo wakati akiwa kazini.

Kachero huyo mwenye namba ya EX F 5421 D/C alitimuliwa kazini Oktoba 28, mwaka jana.

Alimfungulia mashtaka IGP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC) Ernest Mangu akidai kulipwa Sh milioni 26.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza, Eugenia Rwajwahuka, alisema jana kuwa kesi hiyo itakuwa ni kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali Februari 8, mwaka 2018.

“Shauri hili la madai namba 6/2017 litakuja kwa ajili ya preliminary hearing (usikilizwaji wa hoja za awali) mbele ya Jaji, Joaquine De-Mello, Februari 8, mwaka huu kutokana na kuwapo vikao mfululizo vya mahakama kuu vya kusikiliza mashauri mbalimbali,” alisema Rwajwahuka.

Wakili wa Mlalamikaji katika shauri hilo, Deocles Rutahindurwa, alisema mteja wake anadai malimbikizo ya mshahara wa miezi 33 (Sh milioni 26.8), posho ya chakula na malipo mengine ya uhamisho Sh milioni 2, akiwa mtumishi wa jeshi la hilo Mkoa wa Mwanza. Akizungumza na MTANZANIA jana, Misalaba alisema akiwa bado ni mtumishi wa jeshi hilo alisimamishiwa mshahara wake Aprili, 2014 baada ya kuhamishiwa Wilaya ya Ukerewe na Magu kikazi bila kupewa stahiki zake zikiwamo posho za uhamisho na usumbufu na gharama za kufunga mizigo.

Alisema baada ya changamoto hizo alipokea barua ya kuachishwa kazi Oktoba 28, mwaka jana bila kuelezwa kwa kina juu ya hatua hizo.

Misalaba alisema ameamua kuchukua uamuzi huo akiamini hakukuwa na sababu za msingi za kusimamisha mshahara wake na kudai kwamba wapo maofisa wengi wenye malalamiko lakini wanashindwa kujitokeza kudai haki zao.

– PICHA: BENJAMIN MASESE

ELIMU: MKUU wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, akikabidhi vyeti vya ubora na vikombe kwa maofisa elimu na walimu wakuu, vilivyotolewa na Wizara ya Elimu,Sayansi, Teknolojia kwa Mkoa wa Mwanza baada ya kufanya vizuri katika mitihani ya taifa ya sekondari na msingi kwa mwaka 2016.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.