DC aomboleza vifo ajali gari iliyoua 12

Mtanzania - - Kanda - Na ANNA RUHASHA

MKUU wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amesema ajali ya gari lililotumbukia ndani ya Ziwa Victoria na kuua watu 12, imeacha msiba mkubwa katika wilaya yake.

Alikuwa akizungumza juzi katika msiba wa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kata ya Nyampande, Kazungu Mayela.

Alisema kati ya watu 12 waliofariki tisa walikuwa wakazi wa Wilaya ya Sengerema.

Ajali ya gari hilo Toyota Hiace namba T 229 BBW ilitokea Oktoba 9, mwaka huu baada ya kupata hitilafu ya mfumo wa breki na kutumbukia ndani ya Ziwa Victoria eneo la Kivuko cha Kigongo ikiwa na abiria wapatao 15.

“Sengerema tumepata pigo kubwa, tumepoteza watu tisa, wote ni wakazi wa wilaya hii kutoka kata za Nyampende, Busisi, Bitoto na Ibisabageni.

“Tumepoteza nguvu kazi, hivyo tukio hili ni tukio la ajali kama ajali na niwaombe kutolihusisha na imani za ushirikina,” alisema Kipole.

Alisema ajali nyingi hutokana na uzembe au makosa ya binadamu lakini jamii imekuwa ikikimbilia kwenye imani za ushirikina.

Aliwasihi waliofiwa ndugu na jamaa a kumshukuru Mungu na kumuomba kuwajalia nguvu katika kipindi kigumu cha msiba. Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) pia alitoa salamu zake za rambirambi na akisema serikali ya wilaya hiyo imepoteza nguvu kazi ambazo zilikuwa zinategemewa na taifa kwa ujumla. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Makoye Augustine alitoa rambirambi ya kwa familia ya wafiwa na kuziomba familia za wafiwa kutumia muda huo kuwaombea waliofariki dunia.

Akizungumza kwa niaba ya Familia ya Mayela Elia Lukuba alisema familia imepata pigo kwa kuondokewa na baba wa familia, Kazungu Mayela mkazi wa Kata ya Nyampande (43) na kuacha watoto tisa na mjane. DC alitembelea familia zote zilizokumbwa na tukio hilo akifuatana na Mkurungenzi wa Halmashauri Wilaya ya Sengerema, Magesa Boniface, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mwenyekiti wa CCM Wilaya na viongozi wengine.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.