RC awaasa wafanyabiashara kuwa na nidhamu ya biashara

Mtanzania - - Kanda - Na SHOMARI BINDA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Dk. Charles Mlingwa, amewataka wafanyabiashara kuwa na nidhamu kwenye biashara zao.

Amewashauri kufuata ushauri na elimu inayokuwa inatolewa ili kuzifanya biashara zao kukua na kuweza kulipa kodi kukuza uchumi wa taifa.

Alikuwa akifungua mkutano wa wafanyabiashara ulioandaliwa na Klabu ya Biashara ya Benki ya NMB mjini Musoma.

Dk. Mlingwa alisema wafanyabiashara wengi wameshindwa kufanikiwa kwenye biashara kutokana na kutozingatia mambo muhimu ya kukuza biashara kwa kutokufuata ushauri.

Alisema kutokufuata na kuzingatia ushauri wa biashara ni nidhamu mbaya kwenye biashara jambo ambalo litaifanya biashara kushindwa kukua na kushindwa kulipa kodi husika.

RC alisema hatua ya NMB kutoa elimu kwa wafanyabiashara itasaidia kuboresha biashara zao na kufanya kwa faida na kuweza kumudu kurejesha mikopo huku biashara zao zikiendelea kukua zaidi.

“Napenda kuishukuru NMB kwa hatua hii ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara ambayo itawasaidia kuboresha na kukua katika biashara jambo ambalo litasaidia kuwafanya kulipa kodi na kuinua pato la taifa.

“Sina shaka na mipango ya NMB katika masuala ya biashara na kuwainua wafanyabiashara na pale watakapokua wataweza kusaidia katika kuongeza ajira.

“Maana kwenye biashara zao wataajiri watu na sisi serikali tutakuwa tumesaidiwa katika kuongeza ajira,” alisema.

Mkuu wa Mikopo wa NMB, Tom Borgous, alisema hivi karibuni taasisi hiyo itaongeza kiwango cha mkopo kutoka Sh milioni 30 hadi Sh milioni 50 kuwasaidia wafanyabiashara kukuza biashara zao.

Alisema NMB imekuwa ikitoa mikopo kwa wakati kwa wafanyabiashara kusaidia kukuza biashara zao na imekuwa ikipokea ushauri kutoka kwa wateja ambao umesaidia kuboresha utoaji wa mikopo ambayo inaambatana na elimu ya biashara.

Baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki mkutano huo waliishukuru NMB kwa kuwapa elimu ya biashara ambayo imewasaidia kuboresha biashara zao na kuomba elimu hiyo itolewe mara kwa mara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.