NMB yaipa vitanda Hospitali ya Butimba

Mtanzania - - Kanda - Na MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB imetoa msaada wa vitanda 11 vikiwa na magodoro na shuka zake katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ( Butimba) wenye thamani ya Sh milioni 10 kwa ajili ya kinamama wajawazito.

Msaada huo ulitolewa na uongozi wa benki hiyo baada ya kukamilika hafla ya uzinduzi wa tawi jipya la NMB Pamba katika wilaya ya Nyamagana.

Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Abraham Augustino, alisema msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.

“Ni utaratibu wa kawaida kwa benki yetu kutoa sehemu ya faida yake kuwasaidia wananchi ili nao waweze kunufaika na kuona umuhimu wa kuwapo NMB katika maeneo yao,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, aliishukuru benki hiyo kwa kuhakikisha inatoa sehemu ya faida yake katika kuisaidia jamii hususan kwa kutoa msaada wa vitanda hivyo katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ( Butimba).

Vilevile aliipongeza benki hiyo kwa kusogeza huduma za benki karibu kwa wananchi kwa kufungua matawi 32 kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na kufanya sasa kuwa na matawi 211 nchi nzima.

Alisema serikali inaipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo nzuri ya kusogeza huduma za benki karibu na wananchi.

Aliwataka wakazi wa mkoa wa Mwanza kujiunga na kuitumia benki hiyo waweze kuwa na mfumo mzuri wa kuhifadhi fedha utakaowawezesha kupata mikopo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.

“Sasa muache tabia ya kuweka fedha nyumbani, huduma imekwishaletwa karibu, wekeni fedha zenu benki na hii itasaidia kupunguza kesi za kuvamiwa na kuporwa fedha,” alisema.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeweka mikakati mizuri ya kupunguza umaskini kwa wananchi kwa kutumia fursa zilizopo.

Mongella alisema ndiyo maana imekuwa ikiunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali wa maendeleo, zikiwamo taasisi za fedha ikiwamo benki hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.