Mbunge asaidia kutatua kero ya maji Bunda

Mtanzania - - Kanda - Na AHMED MAKONGO

WAKAZI wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, hususan wa Kata za Bunda Stoo, Nyasura na Kabarimu, wanakabiliwa na kero kubwa ya ukosefu wa maji kwa kipindi kirefu, imefahamika.

Hali hiyo huwalazimu kutumia maji ya visimani yasiyokuwa salama na kuhatarisha afya zao.

Habari zinasema wananchi hao hulazimika kutafuta maji umbali mrefu kwa kuyachota kwenye visima vya asili ambavyo maji yake siyo salama kwa afya za binadamu.

Vilevile hutumia muda mwingi kuyachota ikizingatiwa yamekuwa yakitoka kwa kiasi kidogo.

Kwa sababu hiyo, Nbunge wa Bunda mjini, Esther Bulaya, aliamua kutoa fedha zote za mfuko wa jimbo kununua mabomba kukabiiliana na kero hiyo kwa kuwapelekea maji wakazi wa maeneo hayo.

Akikabidhi mabomba hayo juzi kwa niaba ya mbunge huyo, Diwani wa Kata ya Bunda Stoo, Daudi Chiruma, alisema kero ya maji katika mji huo ni kubwa.

“Kero ya maji katika mji wetu wa Bunda ni ya muda mrefu, kufuatia hali hiyo ndiyo maana mbunge wetu ingawa bado anaumwa na anaendelea na matibabu, ameamua kutoa fedha zote za mfuko wa jimbo na kuzielekeza kununua mabomba haya wananchi waweze kupata maji kwa urahisi zaidi,” alisema.

Alisema fedha za mfuko wa jimbo ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi ndiyo maana kwa sasa ameamua kuzielekeza katika mradi wa maji kuwaondolea kero hiyo wakazi wa maeneo hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.