Meya aeleza asivyokuwa na mpango wa ubunge

Mtanzania - - Mkoa - Na WALTER MGULUCHUMA

Nafasi ya udiwani niliyonayo inanitosha na nitaendelea kuwatumikia wananchi -Willy Mbogo

MEYA wa Manispaa ya Mpanda, Willy Mbogo, amesema hana mpango wa kugombea ubunge wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Mbogo, ambaye ni Diwani wa Kata ya Kashauli (CCM), alitoa kauli hiyo jana, wakati akiwahutubia wananchi wa Kata ya Majengo, katika uzinduzi wa kisima cha maji kilichojengwa na Kampuni ya Kuuza Mafuta ya GBP.

Katika maelezo yake, Mbogo alisema amekuwa akizushiwa taarifa kwamba ana mpango wa kugombea ubunge katika Jimbo la Mpanda Mjini, linaloongozwa Sebastiani Kapufi, jambo ambalo si la kweli.

“Napenda kuwahakikishia wakazi wa Manispaa ya Mpanda na wananchi wa Mkoa wa Katavi, kwamba sina mpango wa kugombea ubunge wakati wa uchaguzi mkuu ujao katika jimbo lolote mkoani Katavi.

“Nafasi ya udiwani niliyonayo inanitosha na nitaendelea kuwatumikia wananchi kupitia nafasi hiyo, kwani inanifaa zaidi.

“Yaani, nimekuwa nikizushiwa mara kwa mara, kwamba nina mpango wa kugombea ubunge, wakati sina hata mpango huo.

“Nimeamua kuliweka wazi suala hili kwa sababu limekuwa likijadiliwa na watu wengi na linanisababishia usumbufu pamoja na familia yangu, wakati jambo lenyewe siyo la kweli,” alisema Mbogo.

Pamoja na hayo, alisema ameamua kukanusha taarifa hizo mapema, kwani anaona watu wanazidi kuzisambaza na hivyo kuanza kumletea uhasama na baadhi ya wanasiasa anaoheshimiana nao kisiasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.