Kampeni kudhibiti malaria yaanza Pwani

Mtanzania - - Mkoa - Na GUSTAPHU HAULE

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na shirika linaloshughulikia masuala ya elimu ya afya kwa jamii (TCDC), wameanza kufanya kampeni maalumu inayolenga kutokomeza ugonjwa wa malaria, Mkoa wa Pwani.

Kampeni hiyo, inayolenga kufanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani, ilizinduliwa jana kwenye viwanja vya stendi ya Mailimoja, katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha.

Wakati wa uzinduzi huo, walikuwapo viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Ofisa Maendeleo ya Jamii, Leah Lwanji.

Meneja wa TCDC, Anthony Nacasenga, alisema lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu kwa jamii juu ya kujikinga na ugonjwa wa malaria.

Alisema kwamba, kampeni hiyo imelenga kutoa elimu juu ya kuelimisha jamii kupima kabla ya kutumia dawa, kutumia dawa za malaria kikamilifu, matumizi sahihi ya chandarua na elimu ya wajawazito juu ya kuwahi kliniki ili kumkinga mtoto aliye tumboni.

Alisema kwamba, kampeni hiyo ni mwendelezo wa mikoa mitano ya Tanzania Bara, ikiwamo Kagera, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.