‘Tatizo la saratani linahitaji nguvu ya pamoja’

Mtanzania - - Jamii Na Afya - Na JOSEPH LINO -DAR ES SALAAM

SARATANI ni moja ya ugonjwa ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi hapa nchini na kusababisha ongezeko kubwa la wagonjwa pamoja na vifo. Tishio la saratani limekuwa likishika kasi licha ya kuwapo kwa saratani za aina nyingi, mojawapo inayosababisha vifo vya wanawake wengi duniani ikiwemo Tanzania ni saratani ya mlango wa kizazi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010, inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani kila mwaka ambapo 4,355 kati yao hufariki dunia. Saratani ya shingo ya kizazi huathiri wanawake wengi nchini hususani wenye umri wa miaka 15 hadi 44.

Tanzania ina wanawake zaidi ya milioni 10 walio na umri wa miaka 15 na kuendelea. Wanawake wa rika hilo wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.

Kwa Afrika Mashariki, asilimia 33.6 ya wanawake wote wanasadikiwa kuwa na virusi aina ya Human Papilloma ambavyo ndio visababishi vya ugonjwa huu.

Mtaalamu na mtafiti wa magonjwa ya saratani kutoka taasisi ya T-MARC, Dk. Benjamin Kamala, anabainisha kuwa virusi hivyo huambukizwa kwa njia ya kujamiiana au kugusana kwa ngozi ya mtu mmoja na mwingine.

Dk. Kamala anasema visababishi vingine ni kuanza kufanya ngono mapema kwa wasichana wenye umri mdogo.

“Wanawake wanaoanza kujamiiana wakiwa na umri chini ya miaka 16 wako kwenye hatari baadae kupata saratani ya shingo ya kizazi. “Pia mwanamke mwenye wapenzi wengi au mwenye mwanamume mwenye wapenzi wengi yupo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu.

“Utumiaji wa kondomu hupunguza hatari ya kupata saratani hii, lakini ikumbukwe kwamba kondomu si kinga ya ugonjwa huu,” anasema Dk. Kamala.

Anaongeza kuwa maambukizi ya virusi hivyo vya HPV yanatokana na uvutaji sigara ambapo kemikali zilizopo kwenye sigara huchanganyika na seli au chembechembe za shingo ya kizazi hivyo kuleta mabadiliko katika shingo ya kizazi hatimaye kusababisha saratani.

“Maambukizi mengine yanatokana na utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu, ugonjwa wa masundosundo, lishe duni au utapiamlo, kuzaa watoto wengi, umri mkubwa, upungufu wa kinga mwilini na

uasili wa mtu,” anasema.

Dk. Kamala anasema saratani ya shingo ya kizazi katika hatua za awali haina dalili au viashiria vyovyote mpaka unapopita muda ndipo dalili mbalimbali zinapoanza kujitokeza. Anasema dalili za ugonjwa huu ziko nyingi ila baadhi ni mwanamke kutokwa na damu ukeni ambayo si ya kawaida, kutokwa damu baada ya kujamiana, maumivu makali wakati wa kujamiana.

Dk. Kamala anafafanua zaidi kuwa ugonjwa huu ukishasambaa zaidi muathirika hujisikia hana hamu ya kula, uzito hupungua, muda wote huhisi uchovu, husikia maumivu makali kwenye nyonga na mgongo, maumivu katika miguu, mguu mmoja kuvimba na kutokwa na mkojo au kinyesi kwenye uke.

Kutokana na ongezeko la ugonjwa huu ambao unazidi kuwa tishio nchini, Kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia taasisi yake ya kusaidia jamii ya Vodacom Foundation, imeamua kulivalia njuga tatizo hili ikiwa imejikita zaidi kushirikiana na taasisi mbalimbali za afya kuwaelimisha wanawake kupima afya zao mara kwa mara ili kujua iwapo wako salama.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania na mfuko wa kusaidia jamii wa kampuni hiyo, Rosalynn Mworia, anasema kampuni hiyo imeamua kujikita katika kukabiliana na tatizo hili kwa kushirikiana na wadau wengine baada ya kuona linazidi kuwa kubwa na kusababisha vifo vya wanawake wengi nchini.

Anasema mwaka jana taasisi hiyo ilitoa msaada wa Dola za Kimarekani milioni 87,400 kwa ajili ya kusaidia wanawake waliojitokeza kuchunguzwa na kukutwa wameathirika.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania na Mfuko wa Kusaidia Jamii, Rosalynn Mworia

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.