Wazazi tujifunze kutofautiana na watoto bila kuwaumiza

Mtanzania - - Jamii Na Afya - NA CHRISTIAN BWAYA

MZEE Bayo hana uhusiano mzuri na Masala, kijana wake mwenye umri wa miaka 17. Katika mazungumzo yetu, alinieleza kwa nini hatamani kuendelea na hali hiyo.

‘Nimemfanyia vingi. Ninashangaa kwa nini hatuongei. Hakuna kazi inanichosha kama kuanzisha mazungumzo na huyu mtu. Lakini hatuwezi kuongea kitu kikaeleweka,” alinieleza kwa masikitiko.

Nilitamani kujua kwa nini mzee Bayo anafikiri hawawezi kuongea kitu kikaeleweka. Taratibu alikuna kidevu chake kilichokuwa kimeegeshwa kati ya kidole gumba na vidole viwili vinavyofuata vya mkono wa kiume. Mkono wa kulia ulishikilia kikombe cha kahawa.

“Ninaweza kumwambia kitu kwa nia njema kabisa lakini akanyamaza. Kiburi. Akiamua kuongea basi anaweza nijibu kijinga nikakosa uvumilivu na kujikuta namfokea. Sipendi hali hii,” alinieleza huku akijipepea na magazeti aliyokuwa kayashika mkononi.

Nilimdadisi zaidi kujaribu kujua namna anavyowasiliana na kijana wake huyu. Ilikuwa dhahiri mzee Bayo anatamani uhusiano mzuri na kijana wake. Bahati mbaya, hata hivyo, inavyoonakana hakujua namna ya kuwasiliana na kijana wake hasa pale wanapotofautiana.

Nilipomwuliza anafanyaje ikitokea wametofautiana msimamo na kijana wake alijitetea, “Unajua mimi ni mtu mzima. Naelewa what is best for my child (kilichobora kwa mwanangu.) Ninapoona mawazo yake ni ya kijinga lazima niwe na msimamo.”

Nafahamu hivi ndivyo wazazi wengi tunavyofikiri. Tunafikiri kwa sababu tu mawazo yetu ni sahihi basi maana yake hatulazimiki kujali hisia za watoto. Hata hivyo, tunaposimamia yale tunayoamini ndiyo sahihi, tunajikuta tukitengeneza ufa mkubwa wa mawasiliano kati yetu na watoto. Jambo hili lilijitokeza nilipozungumza na Masala mwenyewe. Sentensi ya kwanza aliyoniambia ilimponyoka kama chafya.

“Baba ni mkali sana. Hajui kuongea kistaarabu. Huwa nafanya kunyamaza kwa sababu najua hata niseme nini kama hajakiafiki kitu, ukimwambia unachofikiri anaweza kukumeza. Mimi hiki kitu kinanikera,” alinilieza.

Kama kuna maeneo yanayoweza kujenga ufa mkubwa wa mawasiliano kati ya kijana anayechipukia na mzazi wake, ni namna sisi kama wazazi tunavyoshughulikia tofauti zetu na watoto wetu. Katika umri wake, Masala anajaribu kujipambanua kama mtu mzima mwenye uwezo wa kuwa na misimamo yake binafsi. Malezi katika kipindi hiki ni lazima yazingatie hitaji hili.

Badala ya kumpa amri asizotakiwa kuzihoji, mzazi anahitaji kujifunza kuonesha uelewa kwamba kijana naye anahitaji kujisikia kuheshimiwa kama mtu mzima. Hata katika mazingira ambayo kijana ni wazi amekosea, ni muhimu mzazi kujali hisia za kijana wake.

Kusikia hivyo, Mzee Bayo alitikisa kichwa kipande kunikatalia. Bila kusubiri nimalize alidakia, “Tuache nadharia hapa. Hebu tuwe wakweli. Unaposema niheshimu hisia zake maana yake unataka nilee makosa…”

Ilibidi nifafanue. Nilimwambia, kwanza ni vyema kumpa kijana chipukizi kama Masala nafasi ya kusema mawazo yake hata kama unajua hayako sahihi. Msikilize hata kama anachokisema huoni mantiki yake. Unapofanya hivyo, kijana chipukizi anajisikia unamjali kama mtu mzima. Amri na maelekezo yasiyohojiwa ni baadhi ya vitu vinavyoweza kuzorotesha mahusiano ya mzazi na kijana wake.

Lakini pia, nilimweleza mzee Bayo, hata pale kijana anapokuwa amekosea, ni muhimu kuweka mbele uhusiano wenu kuliko hitaji lako mzazi kuwa sahihi. Staha ni pamoja na kujua namna ya kumkosoa, bila kumfanya akajisikia kudhalilishwa. Unapomwonesha staha, inakuwa rahisi kumshawishi kijana wako kubadilika kuliko kusisitiza ulivyo sahihi na bado ukajikuta ukiishia kubomoa uhusiano wako na kijana wako. Itaendelea. Blogu: bwaya.blogspot.com, 0754870815.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.